Ajali hizi zitaondoa maisha ya watu mpaka lini

28Jul 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ajali hizi zitaondoa maisha ya watu mpaka lini

WIMBI la ajali limeendelea kuikumba nchi na kupoteza maisha ya Watanzania wengi wakiwamo watoto ambao ni tegemeo la taifa la kesho.

Ajali hizo zimekuwa zikitokea  mfululizo wakati machungu ya ajali zingine yakiwa hayajaisha kwenye mioyo ya watu.

Ajali nyingi zinazotokea uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo ni mwendo kasi na ubovu wa magari.

Mwendo kasi wa madereva umekuwa ukisababisha ajali nyingi kwa sababu linapotokea jambo lolote kwa dharura barabarani, dereva anashindwa kuhimili gari na matokeo yake ajali kutokea na kusababisha vifo.

Ajali iliyotokea juzi na kuondoa maisha ya watoto wetu, wakiwamo wa familia moja, imegusa mioyo ya watu wengi. Mzazi kupoteza watoto wake wote kwa wakati mmoja ni jambo la kuhuzunisha sana.

Watoto wasiokuwa na hatia wanaaga wazazi wao asubuhi kwenda shule, baada ya muda taarifa zinakuja hawapo tena duniani.

Ajali hii inakumbusha iliyowahi kutokea miaka ya nyuma ambayo iliondoa uhai wa wanafunzi wengi na wengine kupata ulemavu.

Serikali pamoja na kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti ajali zisiendelee kutokea, kwa kuwataka wamiliki kuweka vidhibiti mwendo na kufanyia magari yao ukaguzi wa mara kwa mara, lakini hilo pia halija saidia.

Pamoja na Kikosi cha Polisi Usalama Barabarani kufanya operesheni kadhaa za kudhibiti ajali hiyo, lakini hali hiyo inaendelea kujitokea mara kwa mara, sio kwa mabasi ya abiria, binafsi, ya serikali na mabasi ya shule, ajali nyingi zinaendelea kushuhudiwa nchini.

Hivi juzi juzi tu, kulitolewa agizo la kufanyika ukaguzi wa magari yote ya shule yanayobeba wanafunzi na ukaguzi huo ulibaini kuwa mengi yalikuwa mabovu yanayotakiwa kufanyiwa marekebisho na matengenezo.

Hatufahamu kama ukaguzi mwingine ulifanyika kubaini kama agizo la kuyatengeneza lilitekelezwa ili kuepusha ajali kwa watoto wetu.

Taarifa za polisi kuhusu ajali iliyotokea juzi na kupoteza maisha ya wanafunzi, zinaeleza kuwa gari walilokuwa wakisafirishiwa watoto hao lilifeli breki na kuishia kutumbukia kwenye korongo.

Kufeli kwa breki kunamaanisha kuwa gari hilo halikufanyiwa ukaguzi, au kama lilifanyiwa kulikuwa na uzembe wa kuliacha litembee barabarani na kuhatarisha maisha ya watu.

Wakati ajali kama hizi ziliposhamiri miaka ya nyuma kwa mabasi ya abiria, serikali ilibadili utaratibu wa ratiba kwa yaliyokuwa yakisafiri usiku na yote kutakiwa kuanza safari asubuhi. Hii ilitokana na kubainika kuwa baadhi ya madereva waliokuwa wakisinzia na matokeo yake kusababisha ajali.

Tatizo lingine ni madereva kujaza abiria kuliko uwezo wa magari yao, hata inapotokea ajali husababisha wengi kupoteza maisha.

Kuna umuhimu mkubwa wa kufanya ukaguzi kila siku kabla dereva hajaingia barabarani kuhakikisha usalama wa gari lake.

Madereva pia kuwa makini wawapo barabarani kwa sababu wanabeba roho za watu wengine. Wahenga wanasema haraka haraka, haina baraka. Na mwendo kasi hata siku moja haujawahi kumuacha dereva salama.

Tuchukue hatua kudhibiti ajali hizi, tusiendelee kushuhudia vifo vya watu wasiokuwa na hatia kwa sababu ya ajali.

Mungu ibariki Tanzania na atuepushe na janga hili la ajali.