Hongera Simba, Mo Dewji, sasa tunasubiri matokeo

03Aug 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Lete Raha
Hongera Simba, Mo Dewji, sasa tunasubiri matokeo

HATIMAYE Simba SC itakuwa na kikao na mfanyabiashara Mohamed Dewji anayetaka kutoa Sh. bilioni 20 ndani ya Simba ili apate hisa ailimia 51.

Pia alipanga kuifanya Simba kuwa na bajeti ya Sh. bilioni 5.5 kila msimu kwa ajili ya klabu hiyo, ili kuwapiku wapinzani Azam na Yanga.

Katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa Simba uliofanyika Jumapili katika Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam kwa kauli moja ukakubali mabadiliko na uongozi kupitia kwa Rais wake, Evans Aveva ukaahidi kuingia kwenye mabadiliko mara moja.

Na mapema Jumatatu barua mbili zilipishana njia, ya Mo Dewji kwenda Simba – na ya Simba kwenda kwa Mo Dewji.

Simba wamemuandikia barua Mo Dewji kumuita katika kikao cha Kamati ya Utendaji Agosti 15 kujadili naye ofa hiyo, wakati mfanyabiashara huyo naye ameandika kutoa rasmi ofa yake kwa maandishi.

Lete Raha tunapongeza hatua ambayo imefikiwa na pande zote mbili na tunaamini sasa mchakato wa mabadiliko ndani ya Simba umeanza rasmi.

Mo amepania kuirejesha hadhi Simba na pia kuifanya iwe klabu kubwa Afrika. Ameahidi kuifanya iwe na uwanja wake wa kisasa ndani ya miaka mitatu na pia ataleta Kombe la Afrika hapa Tanzania kwa mara ya kwanza.

Mo Dewji ni mpenzi na mwanachama wa Simba, ambaye kati ya 1999 na 2005 alikuwa mdhamini Mkuu wa klabu na akazishawishi pia Simba Cement na benki ya NBC kuwekeza katika klabu hiyo hadi ikafuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 ikiitoa Zamalek ya Misri.

Mo pia amewahi kuwa mdhamini wa Singida United na mmiliki wa African Lyon aliyoinunua kutoka Mbagala Market kabla ya kuiuza kwa mfanyabishara Rahim Kangenzi‘Zamunda’ kutokana na kile alichodai haikuwa na wapenzi.

Ukirejea kwenye hali halisi ilivyo ndani ya Simba hakika kiuchumi ni mbaya na inatarajiwa kuwa mbaya zaidi kuanzia mwezi ujao baada ya kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kumaliza mkataba wao wa udhamini huku wakiwa tayari wamesema hawataongeza.

Maana yake ni kuwa klabu hiyo inahitaji mwekezaji ambaye kwanza atainusuru klabu kuporomoka zaidi, na pili kuifanya isimame imara kumudu tu kwanza ushindani wa ndani – kabla ya kuanza kujiinua upya na kugombea mataji hatimaye kurejesha heshima.

Ndiyo maana leo Lete Raha tunawapongeza uongozi wa Simba na Mo Dewji kwa hatua waliyofikia na sasa tunasubiri kusikia matokeo ya kikao chao cha Agosti 15.