Sekta za kilimo na ufugaji yafaa ziboreshwe kupunguza umaskini

02Aug 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Sekta za kilimo na ufugaji yafaa ziboreshwe kupunguza umaskini

SIKUKUU ya Wakulima na Wafugaji maarufu kwa jina la Nane Nane inatazamiwa kuadhimishwa wiki ijayo, Agosti 8.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alizindua jana maonyesho ya wakulima na wafugaji ikiwa sehemu ya wiki ya maadhimisho ya sikukuu hiyo.

Majaliwa alizindua maonyesho, ambayo ni mahsusi kwa wakulima na wafugaji wa Kanda ya Mashariki.

Kanda ya Mashariki inajumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani na Tanga.

Sikukuu ya Nane Nane inakuja katika kipindi ambacho nchi iko katika vita kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watanzania wanajihusisha na shughuli za kilimo.

Ndio maana kwa miaka mingi kumekuwa na na imani kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa maendeleo ya taifa letu.

Hata hivyo, jambo la kusikitisha kuwa pamoja na sehemu kubwa ya wananchi kujihusisha na sekta hiyo lakini inachangia kwa kiasi kidogo kwenye pato la taifa.

Kilimo kinachangia asilimia 25 tu ya pato la taifa la Tanzania licha ya zaidi ya asilimia 70 ya watu wake kufanya shughuli hiyo.

Ikiwa idadi kubwa ya watu wanajihusisha na sekta hiyo ina maana kwa kiasi kikubwa kilitakiwa kuchangia sehemu kubwa ya taifa.

Pamoja na ukweli kuwa nchi yetu imekuwa na kampeni kubwa za kuinua sekta hiyo lakini bado kimekuwa chini.

Ni ukweli ulio wazi kuwa, idadi kubwa ya wananchi wa Tanzania inaishi vijijini na ndio kwa kiasi kikubwa wanajihusisha na mambo ya kilimo.

Hata hivyo, ni jambo la kusikitisha kuona kuwa sekta hiyo bado imekuwa chini, pamoja na wananchi walio wengi kujihusisha nayo.

Serikali imekuwa na kampeni nyingi za kuinua kilimo cha nchi yetu lakini jambo la kusikitisha bado kimekuwa katika kiwango cha chini,

Mathalani watakumbuka Azimio la Iringa maarufu kwa jina la `Siasa ni Kilimo’ ambalo lilipitishwa mwaka 1974 na chama cha Tanu.

Pia mwaka 1976, serikali ilikuwa na kampeni nyingine iliyoitwa `Kilimo cha Kufa na Kupona’ ambayo lengo lake kiasi kikubwa ilikuwa kumaliza baa la njaa.

Katika utawala wa awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete nayo iliiibuka na kauli mbiu ya `Kilimo Kwanza.’
Tunashauri serikali ije na mikakati madhubuti ya kuinua kilimo kwani kwa kiasi kikubwa itasaidia kupunguza tatizo la umasikini nchini.

Serikali inabidi iongeze nguvu katika kuinua kilimo cha nchi yetu ili kuinua maisha ya watanzania, ambao walio wengi wanategemea sekta hiyo.

Wakati Tanganyika ikipata uhuru mwaka 1961, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema kuwa taifa lilikuwa linaingia vitani kukabiliana na maadui watatu, maradhi, ujinga na umasikini.

Hata hivyo, ni miaka zaidi ya 50, tangu vita hiyo itangazwe lakini bado taifa halijafanikiwa katika vita hiyo.

Serikali ili ifanikiwe katika azma yake ya kuinua maisha ya watu wake ni lazima iwekeze vya kutosha kwenye kilimo.

Kutokana na ukweli kuwa itakuwa inagusa maisha ya walio na hata kupunguza makali ya umasikini unaowakabili.

Katika kipindi hiki cha kuelekea Sikukuu ya Nane Nane tunashauri ni vizuri serikali ikaja na mikakati ya namna ya kuinua kilimo cha nchi yetu.

Mkazo ukiwa kutoa pembejeo kwa wakati, kusaidia upatikanaji wa zana za kilimo za kisasa na pia kutengeneza mazingira mazuri ya masoko ya mazao.

Ikiwa kilimo cha kitainuka ina maana kitatoa ajira lakini kubwa zaidi kitainua maisha ya watanzania walio wengi.