Ofa ya Dewji: Viongozi Simba waweke mbele maslahi ya klabu

31Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Lete Raha
Ofa ya Dewji: Viongozi Simba waweke mbele maslahi ya klabu

KWA mara nyingine tena, mfanyabiashara Mohamed Dewji ametoa ofa ya kuinunua klabu ya Simba kwa Sh. Bilioni 20 ili afanye mageuzi makubwa na kuifanya kuwa klabu bora tena nchini.

Rais huyo wa Kapuni ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL) anataka kununua asilimia 51 ya hisa za klabu kwa Sh. Bilioni 20 na baada ya hapo atatumia bajeti ya Sh. Bilioni 5.5 kwa msimu kwa ajili ya Simba SC, ili kuwapiku wapinzani Azam na Yanga.

Ofa hiyo ya tajiri huyo kijana zaidi Afrika kwa mujibu wa jarida la Forbes, inakuja wakati Simba SC itakuwa na Mkutano wake Mkuu wa mwaka leo Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.

Kwa ujumla Mo amepania kuirejesha hadhi ya Simba nchini na pia kuifanya iwe klabu kubwa Afrika. Ameahidi kuifanya iwe na Uwanja wake ndani ya miaka mitatu na pia ataleta Kombe la Afrika hapa Tanzania kwa mara ya kwanza.

Mo Dewji ni mpenzi na mwanachama wa Simba SC, ambaye kati ya 1999 na 2005 alikuwa mdhamini Mkuu wa klabu na akazishawishi pia Simba Cement na NBC kuwekeza katika klabu hiyo hadi ikafuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 ikiitoa Zamalek ya Misri.

Mo pia amewahi kuwa mdhamini wa Singida United na mmiliki wa African Lyon aliyoinunua kutoka Mbagala Market kabla ya kuiuza kwa mfanyabishara Rahim ‘Zamunda’ Kangenzi kutokana na kile alichodai haikuwa na wapenzi.

Ukirejea kwenye hali halisi ilivyo ndani ya Simba hakika kiuchumi ni mbaya na inatarajiwa kuwa mbaya zaidi kuanzia mwezi ujao baada ya kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kumaliza Mkataba wao wa udhamini huku wakiwa tayari wamesema hawataongeza.

Maana yake Simba SC inahitaji mwekezaji ambaye kwanza atainusuru klabu kuporomoka zaidi, na pili kuifanya isimame imara kumudu tu kwanza ushindani wa ndani – kabla ya kuanza kujiinua upya na kugombea mataji hatimaye kurejesha heshima.

Tukubali ofa ya Mo Dewji imekuja katika wakati mzuri, wakati ambao Rais wa klabu, Evans Elieza Aveva anajua hali halisi ya klabu kiuchumi kuelekea Mkutano wa leo wa mwaka – maana yake anapaswa kuamua kwa maslahi ya klabu.

Wanachama ni watu wa kushawishiwa, kuelimishwa na kutolewa wasiwasi juu ya mpango wa klabu kuuza hisa, ili waafiki na hatimaye klabu kuanza mchakato wa kwenda kwenye zama mpya. Ndiyo maana leo Lete Raha tunasema, kwa ofa ya Mo Dewji, viongozi Simba waweke mbele maslahi ya klabu tu.