Waathirika na familia zao wanasononeka kutokana na unyama wanaofanyiwa watoto na kuwasababishia maumivu makubwa kimwili, athari kisaikolojia na kuvuruga ustawi wao.
Matukio hayo yamekuwa mengi na kila wakati yamekuwa yakiongezeka, mbaya zaidi hata watoto wenye miezi sita wanadaiwa kufanyiwa ukatili huo.
Mathalani, Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi lilimkamata mwalimu wa mafundisho ya dini kanisani, huko Mpanda Mjini, Februari mwaka huu kwa tuhumu za kuwalawiti watoto wanne.
Kadhalika mwezi uliopita baada ya kuibua tuhuma za watoto wanane wenye umri kati ya miaka sita na nane kufanyiwa ukatili wa kingono na mwalimu wao katika shule moja ya msingi iliyopo Kinondoni Dar es Salaam.
Taarifa hizo zilitolewa siku saba baada ya uchunguzi wa kina wa tukio hilo kufanyika.
Haya ni baadhi ya matukio ya karibuni yaliyoripotiwa tena katika mazingira ambayo jamii inayaamini kuwa watoto wapo salama shuleni kwenye uangalizi wa walimu.
Walimu wanaaminika tena wanachukuliwa kuwa ndiyo walimu na viongozi wa watoto wakiwa nje ya familia zao au kwenye mikono ya wazazi na walezi.
Ripoti hizo za polisi zinaweza kuondoa imani ya jamii kwa wahusika ambao walikabidhiwa watoto, kama sehemu ya umma wa Watanzania wakishangaa kuwa inakuwaje walimu wanajihusisha na ukatili huo kwa watoto.
Vitendo ambavyo vinabadilisha maisha ya watoto wa kiume na wa kike na kuwasababishia kuwa ‘viumbe’ wasiokubalika ndani ya jamii kutokana na matendo yanayohusishwa na ‘Sodoma na Gomora’.
Miji hiyo inatajwa katika maandiko matakatifu kuwa ilichomwa na moto wa Mungu kutokana na matendo ya ulawiti.
Walimu, wazazi na hata viongozi wa taasisi za kidini wanatakiwa kukemea uovu huo.
Kama walivyo wengine nami najiuliza jamii yetu inaelekea wapi? Suluhu ya haya majanga ni nini? Je, wazazi na walezi tufanye nini kuwalinda watoto wetu, au tumekwama wapi mpaka wanakumbana na matatizo hayo?
Hakuna mlezi au mzazi asiyemlinda mwanawe, juhudi zinafanywa kuwalinda watoto wetu, lakini wahalifu nao wamekuwa na mbinu nyingi ambazo zimekuwa hatarishi zaidi.
Mfano mwalimu wa dini huko Katavi, anadaiwa kabla ya kuwalawiti watoto hao wanne, alikuwa akiwalaghai wamsindikize kwenda kufanya shughuli za kibiashara sehemu tofauti.
Anadaiwa alikuwa anawabeba kwenye pikipiki yake baada ya kumaliza vipindi vyao vya masomo.
Inasikitisha mno, lakini yameshatokea kikubwa ni kudhibiti matendo hayo kwa kuanza na malezi kwa vijana wetu wakiume ambao ndiyo baba wa taifa la kesho.
Ni lazima kuwafundisha kuhusu ubaya na athari za ulawiti ili wakue wakiwa walinzi wao wenyewe na wa dada zao.
Ili hapo baadaye waendelee kuwa walinzi wa wao wenyewe kama watoto wa kiume, dada zao, wadogo zao na jamii nzima.
Wazazi na walezi kwa upande wao wana jukumu la kuhakikisha mienendo ya watoto wao pamoja na watu au wafanyakazi wanaowaachia kuwangalia ama kuwalea.
Ni muhimu kuwa makini nao na kuwachunguza kutokana na ukweli kuwa walezi (yaya) wengi ndiyo watu wanaotuhumiwa na kesi zinazoripotiwa polisi za kuwalawiti watoto.
Kwa upande wa serikali sheria kali zinahitajika kwa wanaokutwa na hatia ya ulawiti, pengine zilizoko zimekuwa nyepesi ndiyo maana vitendo hivi vya kikatili vimekithiri.
Ni wakati wa kusimama na kutazama nyuma taifa likijipanga tena kudhibiti udhalimu huo.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








