Wazazi kuweni makini na watoto kwa Iddi ijayo

28Apr 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wazazi kuweni makini na watoto kwa Iddi ijayo

ZIMEBAKI siku chache sana, waumini wa dini ya Kiislam nchini Tanzania, waungane wa wenzao dunia nzima kuadhimisha Sikukuu ya Idd El Fitri, ikiwa ni maadhimisho ya kumaliza mfungo mtukufu wa Ramadhani.Kwanza, tunawapongez sana.

Nchini Tanzania kama zilivyo sikukuu nyingine, huwa na shamrashara nyingi, wananchi huadhimisha kwa njia mbalimbali.

Kuna wanaobaki tu majumbani mwao na familia zao, lakini wapo wanaoenda kutembelea ndugu na jamaa. Hapa nchini, maadhimisho ya sikukuu karibu zote hufanana.

Hata hivyo, kwa miaka ya karibuni kumezuka tabia ya baadhi ya wazazi kuwaacha watoto wao kutoka majumbani na kwenda kutembea kwa ajili ya kusherehkea sikukuu, wenyewe husema 'wanakwenda kwenye sikukuu.'

Mara nyingi watoto majirani kuanzia miaka umro miwili hadi 10, wanaocheza pamoja hujikusanya na kuondoka pamoja majumbani mwao, kwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea sikukuu.

Wakati mwingine hao wote huongozwa na mtoto wa miaka 15, ambaye yeye ndiye mlinzi wa wengine. kwa sababu akili yake inaonekana imeanza kukomaa.

Huyo anawaongoza ili wasizozane, kugombana na wakati mwingine kazi yake kubwa ni kuwavusha barabara.

Kuna wakati mpango unaanikiwa, pia wakati mwingine inafeli. Ni kwamba inategemea wanakwenda wapi na kufanya nini.

Tumeshuhudia kuna wakati watoto hao wanashawishiana kwenda kwenye muziki, ambao ni maarufu kama 'disko toto'.

Hiyo ni hatari sana, kwa sababu wakati mwingine watoto wanaenda kuingia kwenye kumbi, ambazo zimeezekwa juu.

Kumbi hizo ni maalum kwa wakubwa tu, lakini watoto wanatakiwa hata kama wanakwenda kujiburudisha kwenye 'disko toto', lakini zinatakiwa ziwe za wazi.

Sehemu zao zinatakiwa ziwe kama zile za michezo ya watoto kama kuendesha farasi, bembea na burudani zingine huwa tunaona ni za wazi, labda pembeni kunakuwa na vizuizi kama vile ukuta, ili waingie na viingilio. Kutokana na hilo disko linatakiwa liwe hata kwenye viwanja vya mpira, kwa sababu juu ni wazi.

Miaka 14 iliyopita, Oktoba 2008, watoto 19 wenye umri kati ya miaka 12 mpaka 17 walifariki mkoani Tabora kwenye ukumbi baada ya kutokea mkanyagano.

Ni 'disko toto' lililoandaliwa kwa sherehe za sikukuu kama hii, mbali na hao kufariki, wengine walijeruhiwa na kulazwa, kwa mujibu wa polisi ilitokana na kukosa hewa wakiwa ndani, hivyo baada ya kutaka kutoka nje kwa pamoja, walianza kukanyagana.

Siyo lazima mpaka makamanda wa polisi waanze kutoa tahadhari kwa wazazi. Usalama wa mtoto zaido uko kwa mzazi mwenyewe.

Wazazi wanatakiwa wawe na watoto wao, badala ya kuwaachia madada wa kazi kutembea nao, huku wao wakiwa wamekwenda kwenye starehe zao zingine.

Na wala hawawabani, kinachotakiwa ni kuwachukua mchana na kuwapeleka wenyewe sehemua ambazo wazazi wataona watoto zao watafurahi, hata kama kwenye 'disko' toto, lakini iwe sehemu salama.

Halafu ukiingia usiku wanawarudisha nyumbani na wao wanaondoka kwenye kwenye starehe za kikubwa. Hiyo itawaepusha watoto kwenda sehemu ambazo si salama.

Kuna baadhi ya watoto kuanzia miaka 15 hadi 17, hawa nao wamekuwa na tabia za kwenda sehemu mbalimbali hatarishi.

Mfano ni kwenye jiji la Dar es Salaam, huwav wanakodisha magari ambayo hufanya vibweka barabarani, wakihatarisha usalama wao na watumiaji wengine.

Huko kwenye fukwe wanakoenda nako ni matatizo matupu. Wanafanya vitu ambavyo si tu havina maadili, pia baadhi wanajilazimisha kuogelea wakati ndiyo mara ya kwanza wanaiona bahari, hivyo wanahatarisha pia usalama wao.

Hawa watoto wakubwa kidogo wanatakiwa kuonywa, kutadharishwa na kuelezwa athari za kitakachotokea watapotoroka majumbani na kwenda huko.