Muungano unaendelea kuwa imara tofauti na nchi nyingine ambazo zilijaribu kuungana lakini zikasambaratika.
Mathalani, mwaka 1981, mataifa ya Senegal na Gambia ya Afrika Magharibi yalitia saini mkataba wa makubaliano wa kuanzisha Shirikisho la ‘Sene Gambia’ au SeneGambia Confederation, hata hivyo hawakufikia malengo baada ya kusambaratika.
Aidha, Ethiopia na Eretria ziliungana mwanzoni mwa miaka ya 1950 ikiwa ni juhudi za kuunganisha makoloni ya Italia , lakini hakukuwa na mafanikio na sasa ni uhasama.
Muungano kutimiza miaka 58 leo si kazi ndogo , kwani ni umri unaozidi nusu karne, angekuwa binadamu ni mtu mzima mwenye wajukuu. Katika kipindi hicho Muungano umeendelea kuwaweka Watanzania pamoja wakiendelea kuwa wamoja bila kuwapo wa Utanganyika wala fikra za Uzanzibari.
Miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kujiri kwenye kilele cha maadhiimisho ya Muungano ni mashindano ya insha kuhusu Muungano kwa wanafunzi wa shule za sekondari ambayo yanatarajiwa kuibua washindi sita.
Washindi watatu watatoka Tanzania Bara na wengine watatu ni kutoka Zanzibar ambao wanatarajiwa kupewa zawadi zao leo.
Maandiko au insha hizo zinawapa fursa wanafunzi kuelezea historia ya Muungano, mafanikio na changamoto zake.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Selemani Jafo, anasema Muungano unapotimiza miaka 58 ni jambo la kujivunia na kuendeleza mazuri yaliyopatikana.
Katika ufafanuzi wake, anasema kuwa lengo ni lilelile la kuelimisha umma hasa vijana, ndiyo maana wameandaa mashindano ya insha kuhusu Muungano kwa wanafunzi wa shule sita za sekondari.
Lakini, pamoja na hayo, ingekuwa ni vyema kuwapo kwa utaratibu endelevu wa mashindano ya kuandika insha kuhusu Muungano, usiosubiri maadhimisho, badala yake yafanyike kila mara.
Utaratibu huo ungepanuliwa wigo wake hadi kwa shule za msingi, wafundishwe wauelewe Muungano, kisha nao wawe wanashirikishwa kwenye mashindano endelevu ya insha kuhusu historia ya Muungano.
Ninaamini hatua hiyo inaweza kuwafanya waelewe umuhimu wa Muungano na kuwafanya wawe miongoni mwa wale wanaouenzi kwa manufaa ya pande mbili zilizoungana na kuzaliwa Tanzania.
Kwa utaratihu huo, inawezekana ikawa rahisi hata wanafunzi wanapokuwa watu wazima wakaendelea kuelezea na kuutetea kutetea Muungano mbele ya umma na kuufanya uzidi kudumu vizazi hadi vizazi.
Ukweli ni kwamba, Watanzania hawana budi kujivunia Muungano huo ambao umewafanya waendelee kuthaminiana kuheshimiana, na sasa sherehe za mwaka huu kinazinduliwa kitabu cha historia ya Muungano.
Kitabu hicho chenye lengo la kuelimisha umma kuhusu Muungano kitazinduliwa leo na Samia Suluhu Hassan, zote hizo zikiwa ni jitihada za kuelimisha umma kuuelewa kwa upana zaidi.
Hatua hiyo inaweza kuongeza uelewa zaidi kwa kuruhusu kitabu hicho kutumiwa shuleni kufundishia wanafunzi wa pande zote mbili ili wawe mabalozi wa baadaye wa Muungano huo ambao tangu mwaka 1964 haujatetereka.
Makongamono ambayo yamekuwa kwenye maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano huo ni sawa, lakini kwenye suala la mashindano ya insha lingetafutiwa utaratibu wa kuhakikisha wanafunzi kuanzia wa vijijini hadi mijini wanalielewa.
Ikumbukwe kuwa hao ndiyo viongozi wa baadaye, hivyo ni muhimu historia ya Muungano wakaielewa wakiwa wadogo badala ya kusubiri wanakuwa wakubwa na kuingia kwenye siasa ndipo wanafundishwa.
Kuwaambia vijana kuwa Muungano ni tunu, wauenzi na waulinde bila kujua historia yake inaweza ikawa vigumu kwao, hivyo ninashauri mashindano ya insha yawe endelevu na ikiwezekana historia yake ifundishwe shuleni.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







