Wamachinga wasipoteze fursa hii waliyopewa na serikali yetu

22Apr 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Wamachinga wasipoteze fursa hii waliyopewa na serikali yetu

SERIKALI na wamachinga wamekutana katika kikao cha pamoja kwa lengo la kuweka mikakati mbalimbali ya kuboresha shughuli zao, ili hatimaye watoke kwenye umachinga wawe na biashara kubwa.

Kikao hicho kilichofanyika hivi karibuni jijini Dodoma, kinaweza kuwa msingi wa kuimarisha biashara yao iwapo wafanyabiashara hao watazingatia na kutekeleza kwa vitendo maazimio waliyofikia.

Baadhi ya maazimio hayo ni Wizara hiyo na SHIUMA kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha mamlaka za serikali za mitaa kupanga na kuweka miundombinu wezeshi katika maeneo ya shughuli za wamachinga.

Hatua hiyo inapaswa kufanyika kwa kushirikisha viongozi wa wamachinga wa eneo husika, kuandaa kanzidata ya wamachinga na wizara kutembelea maeneo ya masoko ya wafanyabiashara hao ili kutatua changamoto zilizopo.

Mbali na hilo, wizara pia inatakiwa kuboresha madawati ya kushughulikia masuala ya wamachinga kwa kushirikiana na TAMISEMI hadi halmashauri, ili kutatua changamoto katika maeneo yao.

Aidha, azimio lingine ni sheria ndogo zinazowahusu wamachinga zinatakiwa kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili wazielewe kirahisi na watimize wajibu wao bila msuguano na serikali.

Kutokana na maazimio hayo, ninaamini kwamba, yatasaidia kupunguza kero ambazo zimekuwa zikisababishwa na wamachinga mitaani, na hivyo kufanya shughuli kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Zainab Chaula aliyeongoza kikao hicho, anawataka wamachinga kushirikiana na serikali kutekeleza maazimio hayo, kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.

Ninaamini kwamba kuyatekeleza, kutaondoa sintofahamu kwenye suala la uhamishaji wa wamachinga kutoka maeneo yasiyo rasmi kwenda katika masoko waliyotengewa na serikali, ambao baadhi yao hawajahama.

Miongoni mwa maeneo hayo ni Mbezi Luis Dar es Salaam, ambako wamachinga wanaendelea na biashara kando ya barabara, juu ya mitaro ya maji ya mvua hali ambayo ni hatari kwa usalama wao.

Sababu kubwa ya kuendelea na biashara katika maeneo waliyoondolewa, wanadai ni ukosefu wa maeneo katika masoko, hali inayowalazimu kuuza bidhaa zao hata katika mazingira hatarishi.

Wakati wakisema hayo, wengine hudai kuwa katika masoko mapya hakuna wateja, hivyo wanaona ni bora waendelee kufanya biashara kule walikoondolewa kwa madai kwamba kuna wateja wengi.

Maelezo hayo yanaweza kutumiwa na mamlaka husika kupata ukweli na kuweka mikakati ya kuhakikisha wamachinga wanafanya biashara zao katika maeneo rasmi waliyotengewa na kuepuka mtindo wa kwenda huku na kule.

Nionavyo, serikali ina nia ya kuhakikisha kundi hilo linapata maendeleo kupitia shughuli zake, hivyo kikao cha Dodoma cha kuwajengea uelewa wa mambo muhimu ikiwamo sheria, kanuni na taratibu za serikali ni cha muhimu.

Cha msingi ni kuboresha miundombinu katika masoko yao ili waweze kufanya kazi vizuri zaidi, kwani wana mchango kwenye ajira na inawezekana ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan akawaweka katika kundi maalum.