Tayari baadhi ya mikoa ya pembezoni mwa nchi kama Katavi, Kigoma, ina semekana bei imeshaanza kupanda. Mafuta yakipanda, mara nyingi mfumuko wa bei hauepukiki.
Wakati hali ikiwa hivyo tumesikia Wamiliki wa Mabasi Nchini Tanzania pamoja na Mamlaka ya Usafiri Ardhini Nchini (LATRA) wakiwa kwenye mchakato wa kutaka kupandisha nauli kutokana na gharama za uendeshaji kupanda, ikiwemo bei ya mafuta.
Kwa jinsi tunavyosikia na hali ilivyo sasa duniani, ni ngumu sana kukataa eti nauli zisipande, kwani huko ni kujidanganya.
Vita imesababisha kupungua hata meli za mafuta kuja nchini, lakini hata huko pia uzalishaji umepungua kutokana na tatizo hilo hilo.
Tunatarajia nauli itapanda, hilo wala halina mjadala kwa sababu hata baadhi ya bidhaa mitaani zimeshaanza kupanda.
Kupandisha nauli kutawafanya wamiliki hao kuweza kumudu gharama za kuendesha na kulinda mabasi yao, si kuweza kuweka mafuta tu, pia kuyafanyia matengenezo ili yawe salama kwa abiria na kuwafanya wasafiri kwa raha.
Pia, wamiliki wataweza kuendelea kupata pesa za kuwalipa madereva, makonda, wakata tiketi, mafundi na wafanyakazi wote wa mabasi hayo na wao kupata faida itakayowawezesha kuendelea kuifanya biashara hiyo ya kusafirisha abiria.
Hata hivyo, chonde chonde tunawaomba kuangalia pia hali za Watanzania kwa sasa jinsi zilivyo.
Wakati wa vikao hivyo vya kupanga bei, waangalie jinsi Wabongo 'walivyochoka', hivyo bei watakayopandisha iwe rafiki na isiwaumize.
Kuna bei ambazo ukipandisha unaweza kufukuza wateja, wakabaki nusu, lakini inawezekana kabisa mtu akapandisha bei ikaendelea kuwa rafiki kwa wateja na akapata faida kutokana na ule wingi wao kila wanapoihitaji bidhaa.
Mfano ni kwamba sehemu nyingi za jiji la Dar es Salaam, nauli ni Sh. 400 na zile za maeneo ya mbali hadi 1000, kwani kwa sasa jiji la Dar es Salaam limepanuka sana, nauli inakuwa kuanzia Sh. 500, na kuendelea hadi hata kufikia Sh. 1,000.
Kama maeneo haya yote ikapandishwa shilingi mia moja, yaani maeneo ambayo daladala zilikuwa zikichukua abiria kwa Sh. 400, ikawa Sh. 500, na Sh 700, ikawa Sh 800, itakuwa ahueni kwa abiria.
Hata kwenye mabasi ya mikoani, kama ikiongezwa Sh. 1000 hadi 2,000 juu ya bei ya awali kutegemea na daraja la basi lenyewe, si mbaya. Mfano kama nauli ya kwenda mkoa fulani ni Sh 20,000, basi ipandishwe angalau iwe Sh 21,000.
Kama nauli itapanda hivi sidhani kama kuna abiria atahisi maumivu au kuathirika na namna yoyote ile kwa kupanda bei, lakini vinginevyo itakuwa ni kumpa mzigo mkubwa Mtanzania.
Hatutarajii sehemu ambayo abiria wanakwenda kwa Sh. 30,000, basi ipandishwe hadi Sh 40,000 hadi Sh 45,000.
Bei kama hizi si rafiki kwa Mtanzania, kwa sababu tayari huko alikotoka anakuwa amekutana na changamoto nyingine nyingi za kununua bidhaa ambazo nazo zimepandishwa.
Lakini, hili hata kwa baadhi ya wafanyabiashara wenye uzoefu na mambo hayo wanajua kuwa ni bora kupandisha bei kidogo ili kuendelea kupata wateja wengi kwa sababu ule wingi wao unaziba lile pengo, kuliko kupandisha sana na kushindwa kupata wateja wengi, kwani badala ya kupata faida, sasa inakuwa ni hasara.
Kuna Watanzania wengi, mfano wakazi wa Dar es Salaam kwa sasa wanaishi mbali sana kutoka katikati ya jiji, kama Goba, Mpiji Magoe, Buza, Kisemvule, Chanika, Chamazi, Boko, Bunju, na sehemu nyingi ambazo zipo mbali na katikati ya jiji kama Kariakoo, Posta, Stesheni na maeneo ya karibu na hayo ambapo mara nyingi ndiyo huenda kutafuta riziki zao.
Hawa kwa kiasi kikubwa ndiyo watakaoathirika zaidi kama bei kubwa zitapadishwa, kwa sababu kwanza mpaka sasa tu nauli wanazotumia ni kubwa mno kwenda na kurudi kwenye usafiri, halafu kuna baadhi hadi wafike majumbani kwao, ni lazima pia wapande bodaboda ambazo nazo nadhani zitakuwa zimepandisha nauli zao.
Hawa ndiyo wa kuhurumiwa zaidi kwa sababu hata iweje, hawawezi kuamua kutembea kwa miguu kwenda kazini na kurudi majumbani, tofauti na wale wa Tandale, Kigogo, Mburahati, Mwananyamala, Kinondoni, Magomeni ambao wenyewe wakiamua wanaweza kuutwanga kwa mguu kwenda kazini kama ni katikati ya jiji.
Tukirudi kwenye mabasi ya kusafiri huko ni mtihani, hakuna anayeweza kufanya lolote kukwepa kupanda basi, labda atumie treni au ndege.
Wamiliki wa Mabasi Nchini, na Mamlaka ya Usafiri Ardhini Nchini (LATRA), wana dhima ya kuwatengenezea Watanzania na abiria wote nauli rafiki ili wasiumie.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








