Hili la kila kaya iwe na choo bora lingefaa iwe la lazima

14Apr 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hili la kila kaya iwe na choo bora lingefaa iwe la lazima

MIKOA ya Kilimanjaro, Iringa na Njombe, imetajwa kuwa vinara wa kampeni ya miaka mitano ya uhamasishaji vyoo bora na kuvitumia, yenye jina la 'Usichukulie Poa Nyumba ni Choo' iliohitimishwa Jumatatu wiki hii.

Kilimanjaro imetajwa kuongoza kwa usafi wa vyoo kwa asilimia 89, ikifuatiwa na Iringa asilimia 87.7 na Njombe asilimia 86, halmashauri zikiwa ni Njombe asilimia 100, Iringa asilimia86.6 na Moshi asilimia 85.

Kampeni hiyo ilianza mwaka 2017 wakati huo kukiwapo asilimia 37  tu ya kaya zenye vyoo bora, lakini sasa zimeongezeka kufikia asilimia 72.1, huku ikielezwa kuwa bado baadhi ya Watanzania hawathamini choo.

Wakati kukiwapo ongozeko la kaya zinazotumia vyoo bora, hali hiyo pia inaelezwa kuwa imesaidia kupungua idadi ya wanaojisaidia vichakani, kutoka asilimia 5.7 na kushuka hadi kufikia asilimia 1.4.

Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akihitimisha  kampeni hiyo ya miaka mitano Dar es Salaam, huku ikielezea utafiti wa  Benki ya Dunia unavyoonyesha.

Kwamba, Tanzania hupoteza Dola za Kimarekani milioni 200 kila mwaka kwa sababu ya magonjwa yatokanayo na uchafu, hivyo anahimiza umuhimu wa kuwa na vyoo bora na kuvitumia.

Waziri anasema choo ni sehemu ya kwenda kutolea msongo wa mawazo na  panatakiwa pawe safi, ambapo anawataka Watanzania kuzingatia ujenzi wa vyoo bora na kuvitumia, huku wakikihakikisha vinakuwa safi wakati wote.

Anafafanua kwamba, kuna awamu nyingine ya uhamasishaji wa ujenzi wa vyoo bora itakayofuata baadaye, hivyo kwa maelezo hayo, akidhani ingekuwa vyema kila kaya kuwa na choo bora ingekuwa ni lazima.

Pia, upo umuhimu zaidi wa wataalamu, ikiwa pamoja na maofisa afya kuhakikisha elimu na uhamasishaji wa kila kaya kuwa na choo bora inaendelea kutolewa zaidi, na upatikanaji wa vifaa vya kutosha na vya bei nafuu vinavyohitajika katika ujenzi na matengenezo ya vyoo bora na nafuu.

Uhamasishaji wa kitaifa wa mabadiliko ya kimwenendo katika matumizi sahihi ya vyoo na usafi wa mazingira ambao unaratibiwa na Wizara ya Afya, unalenga kudhibiti tatizo hilo la ukosefu wa vyoo bora.

Hivyo, ili kukabiliana na changamoto hiyo, jitihada za makusudi zinahitajika katika kuongeza umuhimu na uhitaji wa vyoo bora miongoni mwa wananchi kwa kusisitiza zaidi ujenzi na matumizi sahihi ya vyoo bora.

Mikoa inayojigunduia bado imebaki nyuma katika hilo, haina budi kujifunza kwa nyingine zilizofanya vizuri, kwani vyoo bora vina mchango mkubwa katika kulinda afya za watu na jamii kwa ujumla.

Kiafya, inaelezwa kuwa vinasaidia kujenga uchumi imara.

Hiyo inatokana na kwamba, ukosefu wa huduma hizo katika maeneo ya kazi na majumbani, una madhara ikiwamo punguzaji wa uzalishaji, hivyo umuhimu wake ni mkubwa kuanzia nyumbani hadi sehemu za kazi.

Tumesikia taarifa iliyotolewa na Waziri kuhusu kampeni hiyo ya miaka mitano akielezea mafanikio cha changamoto zake ikiwamo baadhi ya mikoa kufanya vizuri kwenye suala la usafi wa vyoo.

Mafanikio hayo ndiyo yanayonishawishi nishauri mikoa mingne kujifunza kitu kutoka kwa ile iliyofanya vizuri, ili ikiwezekana, ichukue mbinu na  kuzitumia, ili hatimaye kila kaya iwe na choo bora.

Si kuwa na choo bora tu bali na kukitumia, kwani wakati wa kampeni kulikuwapo na taarifa kuwa baadhi ya kaya zinajenga vyoo bora, lakini hazivitumii, kwa sababu ya mambo ya mila na desturi.

Ninaamini kwamba Watanzania wengi wanajua umuhimu wa kuwa na vyoo bora, lakini inasikitisha kuona baadhi katika suala hilo, hawajatoa kipaumbele katika jamii zao kwa sehemu kubwa.

Upo msemo 'Nyumba haikamiliki pasipokuwa na choo' lakini msemo huu ni kama umebaki zaidi maneno zaidi kuliko matendo, hivyo kwa kampeni ya 'Usichukulie Poa Nyumba ni Choo' ingesaidia kuwaamsha.