Ama kweli jamani tumuenzi Nyerere kwa matendo yetu

13Apr 2022
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ama kweli jamani tumuenzi Nyerere kwa matendo yetu

LEO Aprili 13, Watanzania tunaadhimisha miaka 100 tangu kuzaliwa Baba wa Taifa, Rais wa Kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Pamoja na vyeo vyote na nyadhifa mbalimbali nchini, lakini mwenyewe alipenda kujiita zaidi kama Mwalimu, akiwa na maana halisi ya kazi yake kitaaluma ya ualimu.

Nyerere aliyezaliwa Aprili 13, 1922 kwenye kijiji cha Butiama, mkoani Mara, alifariki dunia Oktoba 14 hospitalini nchini Uingereza mwaka 1999 alikokuwa anatibiwa.

Ina maana kama angekuwa hai hadi leo hii, angekuwa anatimiza miaka 100. Nina uhakika kuwa si Watanzania tu ambao watakuwa wanaadhimisha hilo, bali hata mataifa mengine ya nje ambayo kwa kiasi kikubwa uhuru wao ulichangia mno.

Moja kwa moja ni Tanzania chini ya mawazo ya Mwalimu na maneno yake kuwa "Tanzania haiwezi kuwa huru, kama nchi nyingine za Afrika hazijawa huru."

Nchi hizo ni kama Msumbiji, Namibia, Zimbabwe, na Afrika Kusini, huku Uganda nayo ikikumbuka jinsi ilivyoteseka chini ya utawala dhalimu wa Idd Amin Dada, kabla ya kung'olewa chini ya majeshi shupavu ya Tanzania, yaliyoongozwa na Hayati Mwalimu Nyerere.

Tumeona makongamano mbalimbali kukumbuka na kuenzi yale yaliyofanywa na hayati Mwalimu Nyerere.

Kila mtu angependa kuendeleza na kuishi kwa yale ambayo Nyerere aliyafanya kuanzia viongozi hadi watu wa hali ya chini, ingawa wakati mwingine ni ngumu sana.

Kuna wakati Nyerere unaweza kumtafsiri hakuwa na kipawa cha kawaida, achilia mbali akili yake, uwezo wa kupambanua mambo, kujieleza, kutoa hotuba isiyochosha hata akizungumza saa kumi ana ushawishi.

Pia, aliishi kwa kile ambacho alikuwa akikizungumza na si vinginevyo. Hakuwa mtu wa majivuno na kujikweza, licha ya kwamba hakuwa kiongozi anayeheshimiwa nchini Tanzania tu, bali Afrika nzima na dunia kwa ujumla.

Ni Nyerere huyo huyo ambaye kuna wakati alikuwa Mwenyekiti wa Nchi Zilizo Mstari wa Mbele za Ukombozi Kusini mwa Afrika, lakini mavazi yake na utakapomkuta wakati mwingine kijijini kwake Butiama, unaweza kukataa kuwa si yeye.

Viongozi wengi waliomfuata Butiama, walimkuta shambani akilima tena kwa jembe la mkono, kitu ambacho kiliwashangaza wengi.

Halafu vilevile kabla ya kuwakaribisha nyumbani kwake na kusema kilichowapeleka, aliwapa elimu kwanza ya kilimo huko huko shambani ambako mwenyewe alipenda wapelekwe kwanza kumtembelea huko, badala ya kumsubiri nyumbani.

Kiongozi aliyekuwa mfuasi wa siasa ya ujamaa, aliishi kijamaa hivyo hivyo, tofauti na hata baadhi ya viongozi wa baadhi ya nchi za nje ambao ujamaa wao ni kwenye mdomo na kwenye makaratasi, lakini nyuma ya pazia, walikuwa wamelimbikiza mali.

Hadi anafariki, hadi leo hapajawahi kuzuka hata tetesi kuwa alikuwa akimiliki mali za ajabu,, achilia mbali, mali zingine, kampuni au viwanda.

Nyumba alijengewa siku zake za mwisho na hakuishi muda mrefu, akafariki. Hakika alikuwa mjamaa wa kweli.

Kingine alikuwa na utu. Alipenda binadamu wote wawe sawa. Hakupenda hata yule ambaye amemzidi mwenzake kwa kipato amnyanyase mwenzake.
Akahakikisha mwananchi ambaye hana uwezo wa kununua kidonge cha dawa, anatibiwa hospitalini bila matatizo.

Akasomesha watoto wa masikini bure, ambao hata ingekuwaje, kwa uwezo wa wazazi wao wasingeweza kupata elimu walizo nazo sasa.

Wanafunzi hawakulazimika kununua madaftari shuleni, badala yake kila lilipomalizika, mwalimu anatia saini na linakwenda kuchukuliwa stoo, pamoja na kalamu.

Ukitaka kumzungumzia Nyerere, unahitaji kujaza kurasa na kurasa, kwa sababu alikuwa na mambo mengi aliyoyafanya ya kuzungumziwa kwenye uongozi wake nchini, nje ya nchi, na hata shughuli zake zingine baada ya kazi, kama vile kucheza bao, na kuandika vitabu mbalimbali.

Ni kiongozi ambaye taifa la Tanzania limepata bahati ya kujivunia kuwa alizaliwa kwenye nchi yake.
Ni kiongozi aliyewashangaza hata viongozi wa mataifa makubwa, wakiwamo waliompinga na hata maadui zake.

Kinachopaswa kwa Watanzania wote wa ngazi mbalimbali, inafaa tumuenzi kiongozi huyu kwa vitendo, hasa kwa kuwa Wazalendo kwenye nchini yetu kama ambavyo yeye alivyolifanya taifa liwe wakati huo, kiasi kwamba hadi sasa limekuwa kama Taifa la familia moja, lisilo la ukabila wala udini.