Pia salamu hizi zifike mbali kwenye mikasa yote ya ajali za magari, kuanzia Mikumi Morogoro wastani wa wiki moja sasa, hadi jana jijini Tanga. Idadi kubwa ya vifo wastani 20.
Marehemu Ngowi na dereva wake walifariki maeneo ya Mlandizi juzi asubuhi baada ya kuangukiwa na kontena lililokuwa kwenye lori alipokuwa akienda Morogoro Kampasi Kuu ya Mzumbe kwenye kikao.
Nitoe pia pole serikalini, kwa wachumi na wanahabari kwa ujumla, kwani taifa limepoteza mtu muhimu kama Ngowi. Ni msomi aliyetegemewa na ajali iliyomzuru ni kwa namna inayozuilika.
Hilo limeshatokea, lakini hadi sasa bado malori yanatembea na makontena yakiwa hayajafungwa kitu chochote.
Hiyo si mara ya kwanza kwa ajali za aina hiyo kutokea. Hadi leo inaonekana bado hatua stahiki hazijachukuliwa.
Taifa kwa jumla limeshapoteza watu wengi kwa namna hii, kuangukiwa na makontena yaliyobebwa kwenye malori. Ajali hizo zimeshawahi kutokea sana Dar es Salaam na hata mikoani, hasa kwenye barabara kuu ya Morogoro au kuelekea Tanga, Moshi na Arusha.
Ilifika hatua hata abiria wakiwa ndani ya mabasi, wakiona wanapishana au kulipita lori lililobeba kontena, au kwenda nalo sambamba barabara moja, basi wanahisi wako hatarini kufika ahera.
Wakati mwingine wanafika hatua kumpigia kelele dereva kuliacha lipite, au alipite ili mioyo yao itulie. Ni hali inayotaka kujirudia.
Imekuwa kawaida sasa, kushuhudia makutano na malori yaliyobeba makontena makubwa barabarani, yawe yametoka bandarini au vyovyote vile.
Ni makontena yanayosafirisha mizigo kutoka jijini Dar es Salaam kwenda mikoani, baadhi nchi za nje kwenye, hadi majirani kama Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zambia na Malawi, mahsusi ni nchi zisizo na bahari.
Mizigo mingi hufungwa kwenye makontema hudhibitiwa kwa kufungwa ili yasianguke na kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine barabarani.
Wapo wasafirishaji wanaoyafunga katika namna ambayo hayahatarishi maisha ya waendesha magari binafsi, mabasi ya abiria na hata madereva wenyewe wa malori hayo.
Kinachoonekana, baadhi hawayafungi vema kiasi cha kusababisha maisha ya watu wengine kuwa hatarini.
Ni kawaida makontena hayo hutakiwa kufungwa na nati maalum pande zote nne, hasa kwenye kona zake na ikiwezekana kushikizwa na minyororo, kutegemea ukubwa wa mzigo uliopakiwa.
Unaweza kukutana na lori limebeba kontena likiwa limepachikwa tu, bila ya kufungwa nati au mnyororo hali ambayo ni hatari kwa maisha ya watu kutokana na ukweli kinaweza kuanguka wakati wowote na kusababisha maafa.
Wengine hawayafungi kwa madai yanapelekwa eneo la karibu, hivyo wanaona usumbufu kuyafunga na kufungua kwa muda mfupi.
Wanachojali zaidi ni uharaka kuliko athari zinazoweza kutokea, iwapo litateleza na kuanguka.
Mara kadhaa zimetokea ajali za makontena kuanguka na kusababisha maafa, hasa sehemu zenye miinuko, milima, mabonde, na kona kali, kwani makontena huteleza na kwa sababu ni mazito, ama anaweza kuanguka yenyewe, au kusababisha hata lori zima kuanguka.
Wakati mwingine, mtikisiko kwa sababu halijafungwa, husababisha lori kuyumba na kumpotezea mwelekeo dereva.
Kwa kufanya hivyo kunasababisha maisha ya watu, ndani ya lori, watumiaji wengine wa barabara na watembeaji kwa miguu maisha yao kuwa hatarini sehemu yoyote inakopita, kwani lolote linaweza kutokea.
Ni muhimu polisi ikalifuatilia hilo kwa umakini na kuwachukulia hatua kali wote wasiofunga makontena kwenye malori yao, ili kuepusha maafa haya tunayoyashuhudia, ilali yanaepukika. Ni uzembe tu unaopoteza maisha ya watu.
Wamiliki na wanaokodisha malori hayo hawana budi kuhakikisha makontena yanafungwa, ili si tu kuepuka ajali, bali nao kuepuka hasara ya malori yao kuharibika na madhila yanayoambatana na ajali.
Wananchi, pia tuna wajibu kuisaidia polisi kwa kutoa taarifa kama wataona hali hiyo, kwani lisipokukuta wewe litamkuta ndugu, jamaa au rafiki yako.
Mamlaka husika za serikali nazo sasa umefika wakati ziangalie muda wa malori ya makontena kutembea. Ifike wakati yaanze kutembea usiku, muda usio na idadi kubwa ya magari na watembea kwa miguu barabarani.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








