Matatizo mengine ni ya kawaida tu yanayoweza kutatuliwa kwa ngazi ya familia, kijiji, kata, wilaya, au mkoa, lakini utawasikia wananchi hao wakielekeza kilio apelekewe Rais wa Nchi.
Utakuta migogoro ya ardhi, wananchi wanamlilia Rais, mjane kadhulumiwa nyumba naye kilio chake kinapelekwa huko, watu wawili wameuziwa shamba moja, nao wanalalamikia hukohuko kutaka haki yao, ili mradi tu, hadi unashangaa!
Mimi ninavyojua Rais wa nchi siyo mfalme, anayeamua hata kesi za au mashauri ya kawaida.
Tanzania ina mifumo yake iliyowekwa tangu wakati wa Uhuru, wapo mawaziri, wakuu na mikoa, wabunge na wakuu ya wilaya. Nchi hii ina viongozi hata wa kata, vijiji na mitaa.
Waliwekwa kwa makusudi, kuhudumia yanayofanana na upeo huo na mengine mengi. Kazi yao kubwa ni kutumikia wananchi. Pia, wanawaweka viongozi kwenye nafasi zao wawatumikie, iwe wameteuliwa au wamechaguliwa na wananchi wenyewe.
Rais yeye anawategemea hao kutatua matatizo na kero za wananchi waliko. Haijulikani ni kwa nini kwa sasa mambo haya yanajitokeza, tofauti na huko nyuma.
Kwanini hayo yote? Nadhani kuna shida mahali fulani, watendaji wengi hawawajibikii majukumu yao. Au wananchi hawawaamini kiasi cha kilio chao wao wanataka moja kwa moja kisikike kwa Rais.
Mimi binfasi nadhani huenda kumekuwapo na kutoaminika kwa baadhi ya watendaji kwa wananchi, labda kutokana na uamuzi wao ambao wamekuwa wakiamua, kiasi kwamba wakuwa n imani haba kwao.
Pia nafikiri kumekuwapo na uzembe, au udhaifu wa kufuatilia masuala mbalimbali au matatizo mbalimbali yanayohusu wananchi na kuyatatua, tena kwa wakati muafaka.
Labda ni kutokana na woga kutojiamini, na wakadhani tatizo litaisha lenyewe, lakini kumbe linazidi kujilimbikiza hadi leo likizaa hali hiyo inayoliliwa.
Jambo muhimu mbele yetu ni kwamba, watendaji wote kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa na kuendelea kusimama kwenye nafasi zao kisawasawa.
Sidhani tutaendelea kusikia mtu kauziwa kiwanja na wahusika wa serikali, halafu baadaye inaonekana ameuziwa kimakosa, naye analalamika kwa Rais.
Rais ana mambo mengi makubwa ya kufanya, ikiwamo hata kusafiri nchi na nchi kuweka mazingira sawa na ushirikiano na watu wa mataifa mbalimbali duniani, ili uchumi uendelee kukua.
Sasa hili la kutaka awajibikie hata lililoko katika ngazi ya mwenyekiti wa serikali za mitaa, ni kuonyesha kuwa wakati anaendelea kupambania taifa kukuza uchumi, kuna watu hawawajibiki kwa kumsaidia kazi ziliziko ndani ya uwezo wao.
Kwa maana hiyo, nadhani imefikia wakati watu waamke na kuwajibika, kila mtu kwenye nafasi yake aliyowekwa.
Pia imefika wakati baadhi ya viongozi wanaohusika, pamoja na watu wa habari kuwapa elimu wananchi kuhusu itifaki. Inawezekana kabisa, ikawa wananchi wengi hawana elimu hiyo, ndiyo maana wao kila kitu wanalilia wasaidiwe na Rais.
Ni kweli, inawezekana ikaja siku Rais akawasikiliza, lakini wawe wamepitia ngazi mbalimbali na imeshindikana kabisa. Hata hivyo, wakati anatatua ni lazima atauliza huko kote tatizo hilo lilipopita ni kwa nini hakutatuliwa, au ugumu ulikuwa wapi, wakati wao wana uwezo wa kulimaliza kabla ya kufika kwake.
Wananchi inabidi waelimishwe kuwa Rais ndiyo mtu wa mwisho na ndiyo ngazi ya juu zaidi nchini na kwa siku ana kazi nyingi mno kubwa anazopaswa kupitia, kuzikagua, kuzifanyia kazi kwa manufaa na nchi na wananchi wake kwa ujumla, hivyo matatizo mengine wayapeleke kwenye ngazi zinazohusika.
Kwa sababu unaweza kusikia malalamiko ya wananchi, wakati mwingine hawajayapeleka kwenye ngazi yoyote ile, ila wakipata nafasi ya kukutana na vyombo vya habari wanataka moja kwa moja yasikike huko wanakotaka na yatatuliwe.
Wananchi wanapaswa wanajue mgogoro, kesi au tatizo hili kwanza likitokea, linaanza kuripotiwa wapi na kama ikishindikana lipelekwe wapi.
Nadhani hii itapunguza kama si kumaliza kabisa matatizo hayo ambayo kwa miaka ya karibuni yameanza kujitokeza sana nchini.
Watendaji wafanye kazi zao walizozitaka wenyewe kwa kuomba kuchaguliwa na wananchi, au watekeleze kile ambacho wameapa na kuahidi kukitelekeza baada ya kuteuliza, ili kila mtu afanye kazi yake, pia wananchi nao wanatakiwa waelimishwe jinsi gani itifaki inafanya kazi na jinsi gani matatizo au migogoro yao, wapi kwa kuyapeleka.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








