Maadhimisho hayo yanafanyika kila mmoja akimtazama mwanamama ambaye ni mwanajamii, mlezi, mzazi na kiongozi wa familia ambaye kila mmoja atakubali kuwa ni nani kama mama.
Wanawake wa Tanzania nyuma ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan, wamedhihirisha kuwa kinamama ni viongozi bora na hilo linabainishwa na vigezo vingi alivyo navyo Rais.
Sifa mojawapo ya kuwa kiongozi ni kuwa mtumishi mwenye msukumo wa kuwatumikia wale unaowaongoza ili kufikia ustawi bora kwa maendeleo.
Nguzo kuu ya kiongozi mtumishi inayoonekana kwa Rais Samia ni kuwatumikia wengine na kutanguliza maslahi yao.
Jambo zuri zaidi kuhusu Rais ni kuwajibika ipasavyo katika majukumu yake ili kufikia dira na malengo waliyojiwekea Watanzania.
Uwajibikaji kwa kiongozi mtumishi kama Rais Samia si hisani bali wajibu wa msingi katika kusaidia kufikia kwa maendeleo ya wananchi.
Kimsingi, taasisi, jamii au nchi zinazoongozwa na viongozi watumishi kama alivyo Rais hufanikiwa kwa haraka katika kupiga hatua za kimaendeleo katika nyanja zote yaani kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Hii ni kutokana na ukweli kuwa viongozi watumishi huzingatia kuwa nafasi walizonayo ni dhamana kwa ajili ya kuwatumikia watu na si kutumikiwa kama baadhi ya viongozi wanavyofanya kwa baadhi ya mataifa.
Kiongozi mtumishi anatenga muda wa kusikiliza kero za wananchi ili kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu. Rais Samia aliweka bayana msimamo wake mapema kwa wateule na wasaidizi wake kuhakikisha wanatenga siku maalum za kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Alisisisitiza kuwa katika ziara zake akikutana mabango ya wananchi yenye kero ambazo zipo katika uwezo wa kutatuliwa na wateule wake kama wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri, basi atawafukuza kazi.
Hii inathibitisha nia ya dhati ya Rais ya kuhakikisha dhamana aliyopewa ya kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, inafanikiwa bila vikwazo.
Uongozi wa kiutumishi umedhihirika pale Rais Samia alivyoshughulikia changamoto ya watumishi wa umma kutopanda vyeo na madaraka kwa muda mrefu.
Akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deo Ndejembi, anabainisha kuwa tangu serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia iingie madarakani zaidi ya watumishi wa umma 180,000 wamepandishwa madaraja.
Hii imeongeza ari ya watumishi kufanya kazi kwa bidii na kujituma zaidi.Vilevile, kiongozi mtumishi huandaa vikao na mikutano ili kukutana na makundi mbalimbali kujua changamoto zao na kupokea maoni yao ili kuyafanyia kazi.
Juni mwaka jana Rais Samia alizungumza na vijana wa Mwanza katika Uwanja wa Nyamagana kwa niaba ya vijana wote nchini ikiwa ni mwendelezo wa kusikiliza kero za makundi ya watu mbalimbali katika jamii.
Aidha Mei 2021, Rais Samia alikutana na wazee wa Dar es Salaam takriban 900 katika ukumbi wa Mlimani City kwa niaba ya wazee wote akiwahakikishia kuzifanyia kazi changamoto zao kama vile kupata matibabu , kulipwa pensheni, kupata wawakilishi katika Baraza la Madiwani na bungeni.
Halikadhalika, kiongozi mtumishi ana sifa ya kukataa kutukuzwa pale anaposifiwa kupitiliza kutokana na mambo mazuri aliyofanya. Katika sherehe za Jubilei ya miaka 25 ya uaskofu wa Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo la Rulenge-Ngara mkoani Kagera, Askofu Niwemugizi anamshauri Rais Samia kukataa kwa namna yeyote ile kulinganishwa na Mungu.
Akitoa ufafanuzi wa ushauri huo, Rais Samia, anasema kuwa hana tabia ya kutukuzwa wala kulinganishwa na Mungu, anajitahidi kuwa na hekima na uvumilivu wa kusikiliza maoni ya wengine kwani hiyo ndiyo kanuni ya uongozi bora.
“Baba Askofu umeniasa mambo ya kukataa kutukuzwa na mimi nataka nikuahidi mbele ya umma huu kwamba, hiyo si tabia yangu na ninajitahidi kujishusha niwe sawa na wengine, maana utumishi huu kama mpango wa Mungu ulivyo ameniweka hapa niwatumikie na sio kujitukuza kwenu.
Nitajitahidi na Mungu anisaidie kuwa na hekima na uvumilivu na niwe na sikio la kusikiliza yale yanayosemwa na wengine, nashukuru sana Baba Askofu kwa maneno haya” alisema Rais Samia.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








