Andiko langu lilieleza tatizo la ukatili lilivyokumba jamii na katika kupambana na ongezeko la vitendo vya kikatili, moja ya hatua iliyochukuliwa na serikali ni kuunda kamati za ulinzi wa wanawake na watoto kuanzia ngazi ya kijiji, mtaa hadi taifa na zipo kamati 18,186.
Kamati hizi zimepewa jukumu la kufuatilia na kuripoti vitendo vya kikatili ili hatua madhubuti ziweze kuchukuliwa dhidi ya washirika, wanaokiuka utu, ustawi wa watu na haki za binadamu hasa wanawake na watoto.
Mdau muhimu katika mapambano na mauaji na ukatili ni viongozi wa dini, ambao wanaheshimika na wenye ushawishi kwa waumini na jamii kwa ujumla.
Mafundisho ya viongozi wa dini yanasisitiza upendo, kuwa na hofu ya Mungu, kusaidiana, kutii sheria za Mungu na za nchi na kwa ujumla, mafundisho haya yanachangia kujenga jamii yenye kupendana na kuheshimiana.
Kutokana na kukithiri mauaji na ukatili hapa nchini, viongozi wa dini wanao wajibu wa msingi wa kupaza sauti zao katika nyumba za ibada, mikutano ya hadhara, makongamano ya dini na ya serikali, kukemea kwa nguvu zote vitendo hivi vya kinyama na kikatili ambavyo ni kinyume na mafundisho ya Mungu wanayowaeleza waamini wao.
Vilevile, wanao wajibu wa kuelimisha jamii kuwa mauaji na vitendo vya kikatili ni kinyume na sheria, kanuni, taratibu za nchi hivyo kwa kutenda vitendo hivyo si tu kuwa ni kumkosea Mungu lakini pia ni kinyume na sheria za nchi na katiba yake.
Mwaka jana nilihitimu Shahada ya Uzamili ya Sanaa Katika Elimu ya Kikisto (Master of Arts in Christian Education - MACE) kutoka Chuo cha Elam Christian University (ECU) kilichoko Mbeya.
Katika utafiti nilioufanya ili kupata shahada, niliupa kichwa “Mchango wa Viongozi wa Kanisa katika Kujenga na Kukuza Maadili Mema kwenye Jamii-utafiti nilioufanya wilayani Kongwa.” Walioshiriki kutoa maoni yao katika utafiti ule waligusia na umuhimu wa viongozi wa dini kuelimisha jamii kuishi maadili mema, kufanya maombi kwa ajili ya viongozi na taifa.
Aidha, viongozi wa dini kuwa vielelezo katika tabia njema, kukemea na kulaani vikali maovu katika jamii ili kuwa na taifa lenye maadili bora.
Kwa hiyo, viongozi wa dini waendelee kuelimisha waamini kuhusu utii wa sheria za Mungu na za nchi. Katika ibada wakumbuke kuiombea nchi na raia ili watu waache kutenda vitendo vya mauaji na ukatili.
Kukemea mauaji na ukatili ndani na nje ya nyumba za ibada kutasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya kikatili.
Viongozi wa dini wasichoke kupaza sauti zao kwani vitendo vya aina hii ni chukizo mbele za Mungu na vinaharibu amani na utulivu ndani ya jamii. Viongozi wa dini wasisitize juu ya roho njema tulizoumbiwa na Mungu, hivyo roho za kikatili za mauaji na kikatili hazitokani na Mungu bali shetani, ambaye hatuna budi kumshinda kwa kutenda yale yampendezayo Mungu.
Kutokana na umuhimu wa viongozi wa dini katika kusaidia kufanikisha juhudi mbalimbali za kimaendeleo zinazofanywa na serikali, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa wilayani Ngara mkoani Kagera anawakumbusha hilo.
Alipohudhuria sherehe ya jubilei ya miaka 25 ya uaskofu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi, anawapa tena viongozi wa dini jukumu la kukemea mauaji nchini.
Rais Samia anaelezea namna anayokerwa na mauaji yanayoendelea nchini na kuwakumbusha kuwa kazi hiyo ni yao wasiikwepe.
Anataja matukio ya mauaji yanayotokana na watu kuuawa au kujiua akisema. “Askofu Niwemugizi umezungumzia suala zima la mmomonyoko wa maadili, ni kweli watu wako mbali na imani za dini zao, niwaombe sana turudi kwenye imani zetu, nitoe wito kwa viongozi wa dini turudi kwenye imani zetu watu wafuate misingi ya imani, sisi serikali tumeona tutaanza kuwafundisha watoto wetu shuleni maadili kwenye somo la uraia.”
Kutokana na imani kubwa ya serikali kwa viongozi wa dini ni wakati wao wa kusimama katika nafasi zao kwa kusaidia kujenga jamii inayoheshimu sheria za Mungu na za nchi ili kuondokana na vitendo vya mauaji na ukatili.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








