Kauli hiyo ya wiki kadhaa zilizopita, zilipigiliwa tena msumari jana, ikiwa na msisitizo wa kumaanisha ilichokitahadharisha.
Mtendaji Mkuu wa Wizara ya Afya, ambaye ni Katibu Mkuu akatoa msisitizo maalum wa tahadhari hiyo, huku akizinyooshea kidole mamlaka mbalimbali zinazoguswa moja kwa moja na athari hizo, ikiwamo wasimamizi wa umeme nchini, TANESCO, akiwataka 'wakae mguu sawa' na kinachokuja kutokana na masika hayo yaliyotajwa.
Ni kauli ya serikali inayotolewa huku kuna salamu kadhaa zimeshajionyesha katika mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro, na Singida imekwishapata salamu siku chache zilizopita, Dar es Salaam nayo jana ikisalimiwa na mawingu mazito, yalioambatana na mvua za wastani.
Mara nyingi kuna baadhi ya meneo yatapata mvua za kawaida, lakini baadhi yatapata mvua nyingi na kusababisha athari kwa vitu mbalimbali, hasa miundombinu, binadamu na hata mali.
TMA wamemaliza kazi yao ya kuwatangazia Watanzania, sasa inabaki kwa wananchi wenyewe kuchukua hatua kutokana na utabiri huo, huku taasisi husika za kiserikali nazo ni wakati wao wakiwa makini, kufuatilia kinachoendelea.
Mpaka naandika hivi, tayari mvua zimeanza kunyesha. Kwa bahati nzuri zimeanza kunyesha taratibu kwani hatujasikia mahala popote kuripotiwa uharibifu wa mali, miundombinu na hata maafa.
Serikali iliunda chombo hiki, siyo kama lengo lake ni kuwatabiria na kuwatangazia tu wananchi ili wasikie tu basi kama vile kutangaza matokeo ya mpira au michezo mbalimbali. La hasha.
Hata matokeo ya michezo yakitangazwa kuwa watu watafurahia kwa kushangilia na wengine watahuzunika, ila wakijipanga baada ya hapo wanaendaje?
Pesa nyingi zimetumika kuunda chombo hiki, huku kila mwaka kikitengewa bajeti ya uendeshaji, kutokana kodi za wananchi. Yote hayo ni ishara ya serikali kuwapenda na kuwajali wananchi wake.
Kinyume nayo, ingewezekana tu wananchi hawajui kinachoendelea, wanaanza kuona mvua inanyesha bila taarifa, halafu kwa bahati mbaya kama ikiwa kubwa zaidi wanashindwa jinsi gani ya kujiandaa na kujihami.
Kwa maana hiyo, wananchi wameshahabarishwa kuwepo kwa mvua, hivyo kila mmoja afanye ambavyo ataona ni jinsi gani mazingira yanamruhusu kufanya pale alipo, jibu la mwisho iwe kuepuka balaa. Na ndicho serikali inachokitaka.
Inawezekana kabisa kuwa baadhi ya watu wapo kwenye mikoa au majiji mengine nje ya mkoa au jiji lake analoishi na familia yake kwa sababu mbalimbali za kikazi au kibiashara na ana mpango wa kutaka kusafiri siku hizi mbili tatu.
Anaposikia taarifa hii inamsaidia kuwahi kusafiri kurejea kwenye familia yake, kwani iwapo atasubiri zaidi asiweze kufanya hivyo kwa sababu inawezekana njiani kukawa na uharibifu wa miundombinu, hivyo ikamsaidia kuondoka huko aliko mara moja.
Wapo wanaolima, wengine tayari wameshatayarisha mashamba, wameshapanda au vinginevyo. Lakini huu ndiyo wakati wa kilimo, hivyo akisikia masika yanakuja, anajiandaa sasa na mambo mengine ya kilimo, pia mengineyo ya mahitaji yake.
Kuna wale wanaoishi maeneo ambayo wanajua kabisa kuwa inapokuja mvua ni matatizo.
Wanapotangaziwa kuwa mvua inakuja, wanakuwa tayari kwa lolote litakalotokea. Kabla hata 'haijachanganya' wanajua wafanye nini. Kila mtu ana mbinu yake ya kuhakikisha nyumbani kwake kunakuwa salama, muhimu taarifa zimemfikia.
Kuna wanaoishi mabondeni, ni miongoni mwa wanaoonewa huruma zaidi. Hivyo taarifa hizo ni muhimu sana kwao, kwani zinawafanya kuchukua hatua za haraka kukomboa familia zao.
Wanachotakiwa ni kuhama, wakikimbilia kuliko salama.
Kutokana na kupanuka kwa miji na vijiji, halikadhalika kuna ufinyu wa miundombinu kwa sasa, yote hayo ni vishawishi vya mafuriko, majengo kujaa maji si mabondeni tu, bali balaa linasonga mbali kila penye mazingira rafiki, yanayopiganwa na kina TMA na wadau wenzake na kiserikali, hata asasi huru.
Kwa kuwa nipo Dar es Salaam, nitoe mfano, hata maeneo yetu, imekuwa kawaida hata kando ya barabara hivi sasa nyumba zinajaa maji.
Hayo yanatokea, huku baadhi ya nyumba nazo mabati yamechoka, misumari yake imechomoka, kuta hazijiwezi, huku paa zikipewa ahueni ya bati zisipeperuke kwa kuwekewa matairi ya gari mabovu na mawe walau ziendelee kupata huo, lakini ikibaki bado ni hatari, pale hali ya hewa inapobadilika, iwe mvua au upepo.
Tahadhari hii inaelekeza kukumbushwa hata maeneo hayo tajwa.
Kama hapatakuwa salama kwa mvua, basi kuna upepo, au vyote kwa pamoja, huku janga la umeme kupata hitilafu yenye hatari, nayo ikisimama katika nafasi yake.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








