Baadhi ya watoto hao ambao wengi wao wana umri wa kuwa shule ya msingi, husafisha vioo vya magari ya kibafsi kisha kuomba wapewe fedha hata kama hawakuruhusiwa kufanya hivyo na wamiliki wa magari hayo.
Katika mazingira hayo, wakati mwingine hutaka walipwe kwa lazima, na wasipopewa, hudiriki hata kuwamwagia maji machafu madereva wanawake kama shinikizo la kutaka walipwe fedha.
Lakini imekuwa ikidaiwa kuwa wakati watoto wakiwa kando ya barabara wakiomba fedha, wazazi au walezi wao huwa wamejificha maeneo ya karibu wakisubiri kuletwa makusanyo ya fedha kutoka kwa watoto hao.
Ili kumaliza wimbi la watoto hao mitaani, kumekuwapo na jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali za kuwarudisha kwao, lakini bado hazijazaa matunda kutokana na kuendelea kuonekana mitaani.
Hata hivyo, sasa serikali imetangaza kuanzisha mfumo maalumu utakaowezesha kuwaondoa mitaani huku ikiagiza walioko nyumbani kwa wazazi wao au walezi kubakia huko.
Katika kufanikisha hilo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Doroth Gwajima, anasema serikali inaandaa mpango utakaokomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Kwanza tunaipongeza serikali kwa kutangaza mfumo wa kuondoa watoto hao mitaani, kutokana na ukweli kwamba, wanakwama kupata elimu ambayo ingewasaidia kutimiza ndoto zao za baadaye.
Mambo ya ukatili wa kijinsia, yanatajwa kuchangia kuwapo watoto wa mitaani, ambapo waziri anasema serikali ina mpango wa kukabiliana na tatizo hilo na kuwezesha familia za watoto wa mitaani ili zijimudu kwa kipato.
Tunaamini kwamba, kwa utaratibu huo, inawezekana watoto wakapungua mitaani na kubaki kwa wazazi au walezi na kupelekwa shule ili kupata elimu, kwani elimu ni miongoni mwa haki zao za msingi.
Lakini pamoja na hayo, tunadhani ipo haja ya kuweka mipango na mikakati ambayo itahakikisha hakuna mtoto wa mtaani au ombaomba yeyote, kwani baadhi yao ndiyo huwatumia watoto kuomba, huku wao wakiwa wamejificha.
Tunashauri hivyo, kwa sababu uzoefu unaonyesha kuwa kila ombaomba na watoto wao wakiondolewa mitaani na kupelekwa kwao, baada ya miezi michache hurudi na kuendelea na kazi ya kuomba misaada.
Kwa mfano, jijini Dar es Salaam, mara kadhaa viongozi wa serikali wamewahi kufanya jitihada za kuwaondoa ombaomba wakiwamo watoto wanaozurura mitaani, lakini baada ya miezi michache huwa wamerejea.
Hivyo, tunashauri kuwa mfumo ambao umetangazwa na waziri kwa ajili ya kuondoa watoto mitaani, ulete matokeo chanya, kwani inawezekana katika kundi hilo wapo viongozi na wataalamu wa fani mbalimbali wa baadaye.
Kimsingi, tunaona kwamba, watoto hao kudhurura mitaani wanaweza kuiga tabia mbaya ambazo wakati mwingine zinaweza kuwafanya wawe watu hatari wa baadaye, hivyo wangewezeshwa kupata elimu.
Tunatarajia kwamba mfumo huo utarahisishwa kwa lengo la kuwanusuru watoto wetu ili wapate haki ya elimu na kuwa nguvukazi ya taifa ya baadaye badala ya kutumikishwa na kuwa wahalifu.










