Hatua hiyo ni muhimu kwa sababu ushindani ulioko sokoni kuziwania fursa finyu za ajira ni mkubwa, hivyo ubunifu, kujituma, kuwejikea nia na kufikiri zaidi kutatua changamoto ya kazi vinafikiriwa kuwa vitaleta ahueni.
Wakufunzi wa Chuo cha Utalii cha Taifa (NCT), pamoja na wadau wa sekta ya utalii, hoteli wanazungumzia hayo na kuibua mbinu mpya kwa wahitimu wa chuo hicho, kwenye mdahalo kuelekea mahafali ya 19 yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, mwezi uliopita.
Wakufunzi wa chuo hicho, wanachosema ni kwamba hakuna ajira itakayowafuata watu bali wafanye juhudi kuitafuta, na hata kama wakijiajiri itawapasa kuwa wabunifu na shughuli zao kuwa za kipekee ili kukabili ushindani mkubwa sokoni.
Kinachohitajika ni bidii tangu wakiwa masomoni ili kufahamika na kuheshimika kutokana na kujituma. Ukijituma unapata ufadhili wa masomo unaweza pia kutumiwa na mashirika ya ndani na ya kimataifa. Lakini ukipata ajira msomi ni lazima uwe na nidhamu ya kazi ya hali ya juu na kuipenda kazi yako, kwa kuwa wenye elimu wengi wapo mtaani bila ajira.
Wahitimu siyo wa NCT pekee na wengine pia waibue mbinu za kukabiliana na changamoto kazini ambayo ni moja ya mafanikio, ikiwamo vijana kuyafahamu mazingira yao ya kazi, viongozi au mabosi wao pamoja na wateja wao.
Lakini hizi si zama za kukata tamaa ni kupambana hadi kieleweke, leo wengi wa wahitimu hukata tamaa mapema kutokana na ama mazingira magumu ya kazi au hata ukali wa mabosi ofisini, hilo si la kuwababaisha , lazima kujitahidi.
Pia kongamano linashauri kujikita katika eneo moja au kutoa huduma nyinginezo kwani kunamfanya mhitimu kujenga uzoefu na kuwa rahisi kutambulika.
Kwenye kongamano hilo, serikali inawapa neno wahitimu na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, anasema, wanatakiwa kutumia ujuzi walioupata kwa kujiajiri, badala ya kwenda kuwa mzigo kwa jamii na taifa kwa sababu ya kushindwa kutoe elimu kwa kukifanyia kazi kile walichokipata chuoni.
Masanja anasema kutokana na uhaba wa ajira wahitimu hao wasisubiri kuajiriwa serikalini pekee au sekta rasmi ikiwamo binafsi bali wajitumie alisema, "chagua moja kuajiriwa, au kujiajiri, usiende kuwa mzigo kule uendako. Ubunifu ni muhimu. Kwa miaka 60 ya Uhuru, hatujawahi kuwa na vazi rasmi, muwe wabunifu wa vazi hili ili kuitangaza Tanzania kikamilifu."
Kama waziri anavyobainisha fursa zinazohusiana na sekta hiyo zipo kuanzia ngazi za chini, kwenye vijiji, wilaya, mikoa na kitaifa na kwamba changamoto iliyoko sasa ni uhaba wa wataalamu wa kuandaa matukio na hafla mbalimbali, kuibua ubunifu na vitu vinavyovuta wengi na yote hayo yakilenga kujiajiri.
Licha ya serikali kuahidi kuwa itaendelea kuimarisha huduma zinazotolewa na sekta hiyo, ikiwamo mafunzo ya chuo kama cha NCT, ingawa UVIKO-19 umesababisha kuyumba kwa shughuli za kitalii na uchumi, vijana bado wanaweza kuchomoza na kujiajiri.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa NCT, Dk. Shogo Mlozi, anasema idadi ya wahitimu inaongezeka kila siku na mwaka huu wakiwa 541 na kwamba mkakati ni kutoa mafunzo ngazi ya shahada ili kupata wasomi na wajuzi zaidi wa sekta hiyo.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








