Ndiyo, nasema hivyo kwa sababu kuna watu wengine wao wakimwonea mtu wivu, basi kinachofuata ni fitina na mambo mengine yanayofanana na hayo ili kumkwamisha ama kumshusha.
Kwa sasa kwenye soka la Tanzania si siri kwamba upande wa waamuzi unabebwa zaidi na mwamuzi wa kimataifa, Frank Komba.
Hatuwezi kuendelea na kuandika chochote, bila kwanza kumpa pongezi zake, kwani mpaka sasa yupo nchini Cameroon akiwa mmoja wa waamuzi kwenye michuano hiyo.
Ndiye mwamuzi pekee kutoka Tanzania amekuwa akiiwakilisha vema, kwani tangu achaguliwe, hatujasikia chochote kibaya, au malalamiko kuwa amechezesha vibaya.
Wakati yupo nchini Cameroon akiwa mmoja wa waamuzi wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), kwa mara nyingine tena Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limemteua mwamuzi huyo bora kabisa kwa sasa nchini, Komba, kuwa miongoni mwa waamuzi watakaochezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi kati ya Raja Casablanca ya Morocco na Amazulu ya Afrika Kusini, utakaochezwa kwenye Uwanja wa Mohamed wa Tano unaotarajia kupigwa Februari 12, mwaka huu.
Kwa muda mrefu wadau wa soka wamekuwa wakilalamika ni kwa nini wachezaji wengi wa Kitanzania hawaendi kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na badala yake mpaka leo bado watu wanaimba wimbo wa Mbwana Samatta na Simon Msuva, huku baadhi yao wakienda lakini baada ya muda mfupi wanarejea hapa hapa.
Mjadala huu nao uligeuka baada ya wengine kudai hata waamuzi wa Tanzania wamekuwa hawateuliwi kuchezesha michuano mbalimbali ya kimataifa tofauti na zamani ambapo wengi kama kina Hafidh Ally, Dastan Daffa, Manyoto Ndimbo, Leslie Liunda, Ally Juma David, Omary Abdulkadir, Gratian Matovu na wengineo ambao waliipeperusha vema bendera ya Tanzania nje ya nchi kwa kuchezesha michuano mbalimbali ya kimataifa ndani na nje ya nchi.
Tanzania iliheshimika kwa kuwa na waamuzi wengi bora kabisa kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, lakini kwa sasa mambo yamebadilika. Baadhi ya waamuzi wa Tanzania wamekuwa wakichezesha soka kwa namna ambayo unashindwa kuelewa.
Kosa la wazi ambalo wala halihitaji mjadala, na wala hata asiyejua vizuri mambo ya soka na sheria zake, anaweza kutoa uamuzi kama ni penalti, kadi nyekundu au adhabu, wakati haistahili pale inapostahili hatekelezi hilo. Tena inawezekana akawa yupo karibu zaidi na tukio kuliko mtu yeyote, lakini akajibaraguza kama hajaona.
Inashangaza kuona waamuzi wengi sasa wanakubali kutawaliwa uwanjani na wachezaji, badala ya wao kuutawala mchezo. Mwamuzi anaweza kusukumwa mpaka anataka kuanguka na wachezaji, lakini huwezi kumuona anachukua hatua na hasa kama wanaofanya hivyo ni wachezaji wa timu kubwa zenye mashabiki wengi.
Huwezi kuwa mwamuzi bora kama huwezi kuitawala mechi na wachezaji wote kama wanavyofanya wenzetu na badala yake kuwaacha wachezaji wakutawale na kujifanyia chochote wanachotaka uwanjani.
Kwa bahati mbaya sana kwa sasa Ligi Kuu ya Tanzania inaonyeshwa mubashara, hivyo sidhani kama wakubwa wa waamuzi Afrika wanaweza kuwachagua waamuzi dhaifu wa Tanzania ambao wanachezesha kwa woga na kwa hisia, badala ya sheria za soka zinavyotaka.
Nadhani sasa inabidi waamuzi wa Tanzania waanze kubadilika ili kuwe na kina Komba wengi huko kimataifa. Inawezekana rushwa, mapenzi ya timu, woga wa mashabiki, woga wa kukosolewa kwenye mitandao ya kijamii na wachambuzi, ndivyo vinavyowafanya waamuzi kutofanya vema, lakini unapotaka kuwa bora huna sababu ya kuogopa kelele za wasiojua sheria/ kanuni za mchezo husika.
Cha kufanya wao wachezeshe kwa kufuata sheria tu wasiogope chochote. Hata Komba mwenyewe wachambuzi walimsema sana kwenye mechi moja ya msimu uliopita ya Simba na Yanga, alipotoka pembeni kwenye mstari na kuingia ndani ya uwanja, kukimbia sambamba na mchezaji wa Simba aliyekuwa anakwenda kushambulia. Wakati wachambuzi na mashabiki wanamshambulia kwa maneno ya kejeli, kumbe wakaja kuambiwa kuwa ni kanuni mpya ya soka iliyotoka hivi karibuni, kila mtu akakaa kimya. Hongera Komba, waamuzi Tanzania waige mfano wako.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








