TARURA mnaongeza machozi zaidi Msumi

25Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
TARURA mnaongeza machozi zaidi Msumi

NI kama mwezi umetimia sasa tangu kuanza matengenezo ya barabara ya Madale Msumi jijini Dar es Salaam, ikitengenezwa kwa ‘kiwango cha vumbi’

Kinaweza kuitwa kiwango cha vumbi kwasababu njia hiyo inamwagwa vifusi vya mawe madogo ambavyo havisambazwi na kushindiliwa kikamilifu.

Kinachotokea baada ya kusambaza vifusi vya kiasi kidogo na kuacha vurumai barabarani ni kuwaachia watumia barabara zawadi ya vumbi muda wote hasa msimu wa kiangazi na matope msimu wa mvua.

Nirejee kwenye barabara ya Madale Msumi wilayani Ubungo, eneo la njipanda ya Mbopo kwenda Msumi Centre, barabara hiyo imekuwa kero kwa wananchi na kuzidi kuwaongezea kilio.

Kipande hicho cha barabara pengine chenye urefu wa kilomita tatu, kimemwagwa kifusi tangu kuanza mwaka huu lakini, hakijasambazwa wala kushindiliwa kikamilifu.

Matokeo yake ni udongo au kifusi kusambaa pembeni ya barabara na kusababisha adha muda wote mvua zinaponyesha.
Wakati huu wa mvua kifusi hicho kinachojaa pembeni ya barabara zisizo na njia za maji kimesababisha malori ya shehena kama saruji, kokoto, mchanga na magari na vifaa vya ujenzi kunaswa na kukwama.

Aidha, imekuwa kero kwa wanafunzi wanaosoma shule za Goba, Msumi, Madale na Makabe kukwama kwenda shule asubuhi kurudi jioni wakilazimika kubadilisha njia na hata kutishiwa maisha kwa sababu ya utelezi barabarani.

Yote hayo, yanatokana na udongo au kifusi kilichorundikwa kugeuka tope na kusababisha magari kutitia yanapojaribu kupishana.

Inakuwa vigumu kuyakwamua kutokana na tope hilo, hivyo kuchelewesha shughuli nyingi za maendeleo hasa kwa wakazi wanaotumia barabara ya njiapanda hiyo ya Mbopo-Msumi.

Matatizo ya usafiri kwa wakazi wa Mbezi Msumi ni mengi kwa vile ni eneo ambalo kwa muda mrefu lilikuwa nyuma na hivi karibuni kinamama wa eneo hilo walimpatia Waziri wa Maji, Jumaa Awesu, dumu la maji machafu wanayotumia kwa vile sehemu hiyo haina majisafi ya bomba wala visima vya DAWASA.

Aidha, pamoja na maji tatizo la barabara ni kubwa na hata pale Wakala wa Barabara za Miji na Vijijini (TARURA) anapojenga barabara za eneo hilo, malalamiko hayaishi.

Hata sasa, wananchi wanaendelea kuilalamikia TARURA kwa kushindwa kushindilia na kuchonga mifereji ya maji kando ya barabara hiyo na kusababisha usumbufu kila wakati.

Wakazi wa Msumi wanaikumbusha mamlaka hiyo ikamilishe kazi ya kutengeneza kipande hicho cha barabara hiyo kwa sababu kumwaga kifusi bila kukisambaza na kukishindilia kikamilifu ni kuharibu fedha za umma na kukera walipakodi.

Uharibifu kwa sababu hakisambazwi na kushindiliwa matokeo yake ni kukiharibu na kuongeza tena hasara kwa walipa kodi. Lakini haiishi hapo, kukwangua barabara na kuzishindilia bila kuweka njia za maji ni sababu inayoongeza barabara kuharibika kila wakati.

Hili nalo TARURA iliangalie ili ituondolee machozi wana Msumi.

Kwa upande mwingine ingependeza kama serikali ingetengeneza barabara za lami nyepesi badala ya kuendelea na ujenzi wa kukwangua na kumwaga kifusi kila mara, hatua inayotumia fedha nyingi lakini bila ufanisi.

Wakazi wa Msumi wanaomba serikali iwafanyie wepesi kwa sababu mvua zikianza kunyesha mfululizo hasa wakati wa masika maisha na usafiri utakuwa mgumu na kukwamisha shughuli zao kutokana na gharama kuongezeka.

Kuchonga barabara kusionekane kama jambo la kusaidia bali la muhimu kwa maendeleo kwa vile bila usafiri na usafirishaji shughuli zote za kiuchumi zinakwama.