Mabingwa watetezi, Simba Queens, wakaanza kwa kishindo baada ya kuibamiza bila huruma Ruvuma Queens kwa mabao 15-0 kwenye Uwanja wa Mo Arena.
Watani zao wa jadi, Yanga Princess nao hawakuwa nyuma, wakaanza kwa kishindo kwa kupata ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Kwenye Uwanja wa Nyamagana. wenyeji, Alliance Girls walianza ligi kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mlandizi Queens.
Timu ya Fountain Gate Princess iliishikisha adabu Ilala Queens kwa mabao 4-0, kwenye uwanja wao wa nyumbani, wakati katika Uwanja wa Meja Isamuyo, Maafande wa JKT Queens waliisasambua Oysterbay Girls mabao 3-1.
TSN Queens, ikiwa nyumbani, Uwanja wa CCM Kirumba ilikiona cha moto, ilipochabangwa mabao 4-0 dhidi ya The Tigers Queens.
Ni ligi iliyoanza bila mvuto sana kama ilivyokuwa msimu uliopita, labda kutokana na kuwapo kwa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Inawezekana kabisa kuwa msimu huu haikuwa na matangazo makubwa kama msimu uliopita, ambapo baadhi ya mechi zilikuwa za kusisimua.
Tuliona mechi moja ya Simba na Yanga iliyoonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni, ilivyokuwa ya ushindani mkubwa uwanjani na hata nje ya uwanja, mashabiki wakiwa wamefurika kama vile mechi ya soka la wanaume.
Na hii ilileta hamasa kubwa kwa wachezaji wenyewe na kujikuta wakijituma na kuona fahari kuzitumikia timu zao, lakini wakiona soka la wanawake sasa limekuwa na thamani.
Kwenye mechi za mwishoni kuelekea kwenye ubingwa wakati Simba Queens na Yanga Princess zikifukuzana kuwania ubingwa, mashabiki walikuwa wakifuatilia matokeo ya ligi hiyo kwenye televisheni, redio na hata mitandao ya kijamii kujua nani kashinda na yupi mwenye pointi na magoli mengi na hata wanaofukuzana kuwania ubingwa.
Mechi za mwisho wakati Simba ikicheza mkoani, Yanga Dar es Salaam, mashabiki wa soka walikuwa wakiulizana na kujuzana matokeo kwenye mitandao ya kijamii, kiasi kwamba Yanga Princess ilionekana kama itatwaa ubingwa, lakini bao la dakika ya mwisho la Simba mjini Dodoma, likawapa ubingwa.
Kama itakumbukwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan tayari amejitolea kudhamini soka la wanawake kwa klabu Ukanda wa CECAFA baada ya kuona kuwa halikuwa na mdhamini yeyote, huku lile la wanaume likidhaminiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
Kwa sasa klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati ya wanaume na ya wanawake yote yana wadhamini.
Nilidhani sasa hapa Tanzania kampuni nazo zingeunga mkono juhudi za Rais kuinua soka la wanawake kuweka udhamini wao kama inavyoonekana kwenye soka la wanaume.
Tumeona hivi karibuni mgogoro wa baadhi ya kampuni kugombania kuwekwa nembo kwenye bega, kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara wanaume, huku kukiwa na kampuni nyingine pia, lakini kuna uhaba mkubwa wa wadhamini kwenye soka la wanawake.
Shirikisho la Soka nchini (TFF), kitengo cha biashara ni kama vile wanajitahidi kusaka wadhamini kwa wanaume, hivyo wafanye hivyo hivyo kwa wanawake. Kwanza huko hakuna kelele na migogoro mingi, lakini kampuni zinaweza kujitangaza vizuri zaidi kwa pesa ndogo kuliko ambavyo wangefanya kwenye soka la wanaume.
Kuna kampuni ambazo zinazalisha au kutengeneza bidhaa za kinamama na watoto, nashangaa ziko kimya kujitokeza kwenye soka la wanawake.
Nadhani pia hata kitendo cha biashara ni wakati wa kuzifuata kampuni hizo na kuzieleza na kuzishawishi zitanufaika vipi na wadhamini ligi hiyo, huku pia wakijitahidi kuitangaza ligi hiyo kwa kuonyeshwa kwenye TV, hata kama ni kwa baadhi ya mechi hasa za Simba Queens, au Yanga Queens.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








