Rais John Magufuli aliwataka kwenda kufanya kazi akiwaeleza kuwa wasimamie mabadiliko ambayo serikali yake imeyaanzisha na kwamba kama wataona kuna mtu ni kikwazo katika kufikia visheni ya serikali, basi wawaweke pembeni wakiwamo makatibu tarafa na maofisa watendaji wa kata.
Rais alisema chini ya Serikali ya awamu ya tano kitakachoangaliwa sio uzoefu bali uwezo wa mtumishi kufanya kazi na kutoa matokeo. Pia aliwaagiza wakurugenzi hao kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali ikiwamo matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs). Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliwataka wafahamu wajibu wao kisheria na kikatiba na kwamba wao sio watawala bali ni watumishi wa umma, hivyo wahakikishe kwamba wanafanya kazi kwa kushirikiana na madiwani pamoja na kusoma alama za nyakati.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliwataka wafahamu majukumu yao na kuwa waaminifu na waadilifu. Pia washirikiane na wakuu wa wilaya, mikoa, wakuu wa idara na kamati za ulinzi na usalama za wilaya. Kadhalika aliwataka kusimamia watumishi wa halmashauri pamoja na kutembelea maeneo yao na sio kukaa ofisini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki, aliwataka kusimamia sheria ya manunuzi ya umma na kuhakikisha halmashauri zao zinapata hati safi pamoja na kudhibiti watumishi hewa kwa kuwa halmashauri zinaongoza kwa kuwa na watumishi hewa kwa asilimia 90. Wakurugenzi wa halmashauri ni watu muhimu kama alivyosema Rais Magufuli jana, kwa kuwa halmashuri zinawagusa wananchi wengi kutokana kuwahudumia moja kwa moja.
Halmashauri ndizo zinazosimamia miradi yote ya maendeleo pamoja na utoaji wa huduma za jamii moja kwa moja kwa wananchi kama elimu, maji, afya na barabara. Hata hivyo, halmashauri nyingi katika miaka ya karibuni zimekuwa zikitoa huduma mbovu na zisizokidhi matarajio ya wananchi. Hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na viongozi na watendaji kutotimiza majukumu yao ya kukusanya mapato sambamba na vitendo vya wizi, rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
Hali hiyo imesababisha halmashauri zetu kubatizwa jina la ‘mchwa’ wanaotafuna fedha za halmashauri. Kimsingi, heshima ya halmashauri zetu imeshuka kutokana na sababu hizo. Sababu kubwa ambayo tunadhani imechangia halmashauri nyingi kugubikwa na ufisadi ni mfumo uliopo ambao unawafanya watendaji wakose udhibiti kutokana na kuwajibika moja kwa moja kwa wizara zao. Watendaji hao wameazimwa na halmashauri kutoka wizarani, hivyo, mishahara na maelekezo kwao ni kutoka wizarani.
Katika hali hii siyo rahisi Mkurugenzi ambaye naye ameazimwa na halmashuri kutoka Tamisemi akawa na uwezo wa kuwadhibiti. Madiwani nao hawana mamlaka ya kuwadhibiti na ndiyo maana pale yanapotokea matatizo, inakuwa vigumu kuwawajibisha.
Hata hivyo, tumepata faraja kusikia Rais Magufuli akiwapa mamlaka wakurugenzi kuwaweka pembeni wale wote watakaoonekana kuwa kikwazo katika visheni ya Serikali yake na bila shaka hata watendaji wakuu wa halmashauri wataguswa na siyo makatibu tarafa na watendaji wa kata na vijiji tu kwa kuwa hakuna vigogo wa wizara watakaowalinda. Ni matumaini yetu kuwa maelekezo waliyopewa na viongozi wakuu wa nchi watayazingatia na kubadili sura na utendaji wa halmashauri zetu.










