Ni fursa sasa kwa Tanzania kunufaika ushirikiano na India

12Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ni fursa sasa kwa Tanzania kunufaika ushirikiano na India

WAZIRI Mkuu wa India, Narendra Modi, juzi alihitimisha ziara yake ya kiserikali nchini, ambayo pamoja na mambo mengine, alikukutana na kufanya mazungumzo na viongozi waandamizi wa Serikali walioongozwa na Rais John Magufuli.

Katika ziara hiyo ambayo Modi aliongozana na ujumbe wa wafanyabiashara 50, Tanzania na India zilionyesha nia ya kukuza ushirikiano wa biashara na sekta zingine za kiuchumi na kijamii, kwa kukubaliana kuanzisha kiwanda cha kutengeneza pikipiki na bajaji nchini ili kukuza uchumi na kutoa ajira kwa watu wengi na vilevile ziliazimia kushirikiana katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kuimarisha usalama wa nchi na ukusanyaji wa mapato.

Akizungumzia makubaliano hayo, Rais Magufuli alisema Tanzania imekuwa mnunuzi wakubwa wa pikipiki na bajaji kutoka India, hivyo kuna haja ya India kuja kuwekeza nchini kwa kujenga kiwanda kitakachokuwa kinatengeneza pikipiki na bajaji.

Mbali na pikipiki na bajaji, Tanzania pia ni mnunuzi mkubwa wa magari aina ya tata na Leyland kutoka India. Eneo lingine ambalo Tanzania iliialika India kuja kuwekeza ni sekta ya madini, kwa kuwa Tanzania ina utajiri mkubwa wa madini ya kila aina ikiwamo Tanzanite ambayo inapatikana nchini pekee.

Ziara hiyo inaashiria neema kwa Tanzania kutokana na India kukubali kuipatia Tanzania Dola milioni 500 (Sh. trilioni 10.074) kusaidia miradi ya maendeleo sambamba na ahadi ya Modi ya kuisaidia Tanzania mashine ya kupimia magonjwa ya shinikizo la damu katika Hospitali ya Rufani ya Bugando, kukubali kuisaidia Dola milioni 178 (Sh. bilioni 382.4) kuanzisha wa mradi wa maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani pamoja na utoaji wa mkopo wa Dola milioni 92.8 (Sh. bilioni 197.66) kwa ajili ya usambazaji wa maji.

Katika ushirikiano huo wa kihistoria, thamani ya bidhaa zinazouzwa kutoka Tanzania kwenda India kwa mwaka zimeongekeza na mwaka 2009 ilikuwa ni dola za Marekani milioni 187 (Sh. bilioni 197.66) na sasa zimefikia Dola bilioni 1.29 (Sh. trilioni 2.148).

Tanzania pia itaendelea kupata fursa ya kuiuzia India mazao jamii ya kunde ambayo India inayahitaji kwa wingi. Mwaka jana Tanzania iliiuzia nchi hiyo tani 100,000 na kupata Dola milioni 200. India inahitaji tani zaidi ya milioni saba.

Tanzania kadhalika imeiomba India kuwekeza nchini katika sekta ya afya kwa kujenga kiwanda cha kutengenezea dawa za kutibu moyo, figo na utengenezaji wa vifaa tiba. India pia imekubali kushirikiana na Tanzania katika nyanja za elimu, biashara, uwekezaji, miundombinu, madini na gesi.

Sisi tunaona kwamba sasa ni wakati mwafaka kwa Tanzania kuchangamkia fursa ya ushirikiano na India kwa sababu India ni miongoni mwa mataifa machache mapya ambayo yanaendelea kwa kasi kiuchumi na kiteknolojia duniani, kwa kuzingatia kuwa zimekuwa katika ushirikiano wa kibiashara kwa miaka mingi na sasa umeongezeka na kufikia thamani ya Dola bilioni tatu ( Sh. trilioni 6.44) kwa mwaka.

Ni matumaini yetu kuwa ushawishi walioufanya Rais Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa India ni utawavutia kuja kuwekeza nchini. Majaliwa aliwaeleza wafanyabiashara wa India kuwa kuna fursa nyingi za kuwekeza kwenye sekta ya mifugo hasa katika uanzishaji wa ranchi za mifugo, usindikaji wa maziwa na nyama, usindikaji wa ngozi na utengenezaji wa bidhaa za ngozi.

www.guardian.co.tz/circualtion