Safari hiyo si ya mchezo kwa kuwa ni lazima klabu zijipange na kufanya maandalizi ya nguvu na ya muda mrefu.
Tayari zipo klabu ambazo zimeanza mazoezi kuelekea kwenye msimu mpya wa ligi na kwa uchache klabu hizo ni pamoja na Simba, Azam FC, Ndanda FC, Mbao FC pamoja na mabingwa yanga ambao maandalizi yao ni ya muda mrefu kutokana na ushiriki wao katika mashindano ya kimataifa msimu huu.
Nipashe tunawakumbusha viongozi wa klabu, mabenchi ya ufundi kujipanga na kuanza maandalizi sasa kama kweli wana lengo la kufanya vizuri msimu ujao wa ligi.
Tunawakumbusha kwamba kwenye soka hakuna matokeo mazuri yanayopatikana bila kuyatolea jasho na kujituma hasa katika maandalizi.
Kwa klabu ambazo zimepanda daraja ni lazima zijipange na kujiandaa kikamilifu na ligi hiyo kwa kuwa inahitaji maandalizi mazuri na ya muda mrefu na vile vile kuwa tayari kukabiliana na changamoto za ligi hiyo kutokana na ushindani unaotokana na kushirikisha klabu kongwe, vinginevyo zitajikuta zikirudi zilipotoka mwishoni mwa msimu.
Siku zote maandalizi ya zima moto hasara yake inaonekana katikati ya msimu au mwisho pale wachezaji wanapochoka na kujikuta timu ikifanya vibaya na hataka kama itakuwa inaongoza ligi itaanza kuporomoka.
Mifano hiyo ipo na ni vizuri kwa klabu zote za ligi kuu zikiwamo zile zilipanda daraja msimu huu kujifunza kwa wale waliowatangulia.
Mkoa wa Tanga lilikuwa na klabu tatu kwenye ligi msimu uliomalizika hivi karibuni na kuwa mkoa wa pili kwa kuwa na klabu nyingi kwenye ligi, lakini kwa sasa tunazungumza mengine, baada ya kushuhudia klabu zote zikiteremka daraja na msimu ujao mkoa huo hautakuwa na klabu yoyote kwenye Ligi Kuu.
Ukiangalia kwa undani pamoja na migogoro, lakini sababu nyingine lingine iliyosababisha klabu hizo kufanya vibaya na kushuka daraja ni maandalizi ya zima moto waliyoyafanya kwenye maandalizi ya ligi hiyo.
Hilo linapaswa kuwa fundisho kwa klabu nyingine katika kuelekea kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu.
Tunawapongeza Simba, Azam, Yanga na klabu nyingine zilizoanza maandalizi mapema, ukiwamo usajili wa wachezaji.
Tumesikia Simba imekwenda kuweka kambi ya wiki tatu mkoani Morogoro, Azam wameanza maandalizi yao kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Azam Complex na Yanga ambao wamekuwa kwenye mazoezi na mechi tangu kumalizika kwa Ligi Kuu wakiendelea na mazoezi yao kwenye uwanja wa Boko Veterans huku pia Ndanda FC wakitangaza kuanza mazoezi wiki hii mkoani Mtwara.
Wengine wanapaswa kuiga mfano wa klabu hizi na hata klabu zingine zenye migogoro wa uongozi kama Stand United kuhakikisha wakaweka tofauti zao pembeni na kuunganisha nguvu kwenye maandalizi ya timu zao.
Mpaka kufikia leo umebaki mwezi mmoja na siku chache kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu, hivyo klabu zitumie muda uliobaki kujiandaa vyema.
Kama kila klabu au asilimia 85 ya klabu zote zikiwa kwenye ubora, Nipashe tunaamini wadau wa soka wataona ligi nzuri na yenye ushindani zaidi ya msimu uliopita.
Tunazitakia kila la heri klabu zote zitakazoshiriki Ligi Kuu maandalizi mema na tunatarajia ligi yenye ushindani mkubwa.










