Wenye ulemavu miguu wahakikishiwa hawatakwama kuendesha magari

28Mar 2023
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wenye ulemavu miguu wahakikishiwa hawatakwama kuendesha magari

JOSEPH Sanga ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akisoma shahada ya Uhandisi Mitambo kuanzia mwaka 2019.

Anapomaliza chuo anakuwa mjasiriamali, akifanya ubunifu wa mashine na vifaa vinavyotatua changamoto nyingi zikiwamo za wanaoishi na ulemavu.

Ni kuwatengenezea kifaa rafiki kwenye magari yao ili waweze kuyaendesha kwa wepesi badala ya kukwama kutumia vyombo vya moto na kuendelea na maisha yao kama watu wengine.

Sanga baada ya kumaliza chuo anajiunga na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuendeleza ubunifu na kwa ushirikiano na wenzake walibuni mashine inayofungwa kwenye gari ili kumwezesha mlemavu, aliyeumia au kupooza miguu, kuendesha gari kwa mikono pekee.

Nipashe inakutana na Sanga jijini Dar es Salaam, kwenye jukwaa linaloandaliwa na Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) linalowaleta pamoja waandishi wa habari za sayansi na teknolojia na watafiti ili kuwajengea uwezo wa kufikisha matokeo ya kazi zao kwa jamii. Anasema kifaa hicho kinamwezesha mwenye matatizo ya miguu kuendesha gari kama alivyokuwa hapo awali kabla ya kupata matatizo, akiongeza kuwa ni moja ya njia wanayotumia kumsaidia aliyepata ajali kuendelea na shughuli zake ikiwamo kuendesha gari.

“Kwa sababu wapo waliopata ajali wakati wakiwa wanafanya shughuli za kuendesha magari au bajaji nimebuni kifaa ambacho kinatatua changamoto ya mlemavu wa miguu, kuendesha,” anasema Sanga.UBUNIFU ULIVYOJIBU

Sanga anaeleza kuwa kifaa hicho ni wazo la muda mrefu na aliliendeleza kwa kubuni njia mbalimbali za kulifanya liwe uhalisia, ili kuwatafutia ufumbuzi wenye ulemavu wa miguu, ili watumie mikono kuendesha magari.

“Nilianza kutengeneza vifaa vya kuunganisha kabla ya kukiunda kifaa au mashine yenyewe na hili nililifanikisha kwa sababu ni kitu ambacho nilifikiri muda mrefu kiwe jibu la watu hawa waliokuwa wanaendesha gari lakini wameacha kwa sababu ya ulemavu,” anafafanua zaidi.Anaongeza kuwa vifaa alivyotumia kuunganisha kupata mashine hizo ni vyuma ambavyo vilianza kuungwa katika mfumo unaomwezesha dereva huyo kutumia mkono na kushika vifaa ambavyo vingeguswa kwa miguu.

Aidha, anasema kifaa hicho kinawekwa kwenye kiti au siti ya dereva ili kukanyaga mafuta na kushika breki kwa kutumia mikono badala ya miguu, na kinaweza kuwekwa na kutolewa kwenye gari bila kuleta madhara kwa mtumiaji.

“Hivyo asubuhi anaweza kutumia mwenye ulemavu kuendesha lakini mchana asiye na changamoto za mahitaji maalumu akikitoa na kuendelea na kazi. Nilikiunda kwa kushirikiana na vijana wenzangu wawili, kilikaguliwa na Jeshi la Polisi kama ni salama, baadaye kikafikishwa Shirika la Viwango (TBS), kwa ajili ya kuanza kutoa huduma rasmi.”Sanga anaongeza kuwa kifaa hicho kinatumiwa kwa magari ambayo ni ‘automatic’ ambayo hubadilisha gia na breki peke yake unapokanyaga mafuta, wakati ile manual hutamkwa ‘manyo’.inayotumia mkono unashikilia na kubadilisha gia na breki kwa mkono.

 

Anasema kwa usimamizi wa SIDO au kuatamiwa na shirika hilo anafanya ubunifu wa mashine na vifaa vidogo vidogo kwa ajili ya kutatua changamoto zilizopo ndani ya jamii.

 

GHARAMA/USALAMA

Sanga anataja gharama ya kukifunga kwenye gari kuwa ni Shilingi  600,000 na kufafanua kuwa ni salama kwa watumiaji wa magari, akisema hakina tofauti na mtu anayetumia vifaa vingine halisi vya magari, akiwahakikishia watumiaji kuwa dereva anaweza kukanyaga breki, mafuta na kuendesha gari bila changamoto.

“Kifaa hiki kikifungwa kwenye gari mtu akiwa nje hawezi kuona kuna utofauti wa kutumia mguu na mkono kuendesha gari. Namna ya kuendesha, unaweza kutumia mkono wa kulia au kushoto kutegemea na uhitaji wa mtumiaji. Wengine wanatumia kushoto si kulia hiki kifaa kinaweza kufungwa upande ambao dereva anaweza kuutumia,” anasisitiza.Anafahamisha kuwa mashine hiyo haitumii mafuta wala umeme ili kufanya kazi bali bolti  ili kukifunga na haihitaji matengenezo ‘ service’ kwa sababu si ya mafuta wala haigharimu chochote kwenye gari na kuwashauri wenye ulemavu kuzitumia.

Mbali na kifaa hicho Sanga alibuni kifaa cha kunawa mikono kinachokanyagwa kwa mguu ili kupata sabuni na maji bila kushika bomba wala chpa ya sabuni ya maji, akifanya hivyo kabla ya kuwapo kwa tishio la UVIKO-19, na kwamba baada ya kukitengeneza wengi walikielewa lakini hawakuwa tayari kukinunua ila baada ya kutokea UVIKO-19 alizalisha vingi kwa ajili ya kuwekwa kwenye ofisi na maeneo ya mikusanyiko ili watu kunawa na kujikinga na maambukizi ya vizuri hivyo.Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Nungu, anasema wanashirikiana na wabunifu hao kujenga ili watimize bunifu mbalimbali katika kutoa majibu ya changamoto zilizopo ndani ya jamii.“Tumewezesha wabunifu wengi kutimiza bunifu zao ambao kwa sasa ni walipakodi wakubwa nchini kama Maxcom Afrika ambaye alipita hapa na sasa yupo Msumbiji na tumeendelea kuwezesha nyingine nyingi,” anasema Dk. Nangu.Mwisho

 

Top Stories