Chama cha Madaktari chaunga mkono vitita vipya vya NHIF

01Mar 2024
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Chama cha Madaktari chaunga mkono vitita vipya vya NHIF

VITITA vipya vya matibabu vilivyotangazwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) vinaanza kutumika leo, Chama cha Madaktari nchini (MAT) kimeviunga mkono.

MAT wamesema kuwa wanaunga mkono kuanza kutumika vitita hivyo vipya, wakisema wako tayari kutoa huduma kwa wanachama na mfuko huo.

Chama hicho pia kimethibitisha kushirikishwa na kushiriki kutoa mapendekezo yake katika kuboresha upungufu kiliokuwa kinaona ulipaswa kufanyiwa kazi kwa kuboreshwa.

Rais wa chama hicho, Dk. Deus Ndilanha, katika tamko rasmi la MAT jana, alisema chama hicho kinaunga mkono yale yote yaliyopendekezwa na kamati iliyohusika na maboresho ya vitita vya NHIF.

"Kwanza, tunaunga mkono mapendekezo ya kamati na sisi MAT tunaamini kamati ilikuwa huru na imeenda kwenye uhalisia, na kwa msingi huo yale yote ambayo wameyapendekeza tunayaunga mkono," alisema Dk. Ndilanha.

Alisema mapendekezo yote yaliyowasilishwa na chama hicho kwa kamati yalifanyiwa kazi.

"Nitoe pongezi kwa maboresho ambayo mfuko umeyafanya, na ni baada ya mazungumzo. Ninafikiri wananchi wanakumbuka kwamba mwaka jana mwishoni, mfuko ulitoa kitita na ukasema kwamba una mpango wa kufanya maboresho na kitaanza kutumika mwaka huu.

"Sisi kama MAT tulipata hiyo nafasi baada ya Waziri wa Afya kuunda kamati huru ambayo sisi tulipata nafasi tukaenda kupeleka hoja.

"Na kwa kweli kwa asilimia kubwa yale ambayo madaktari walikuwa wanayapigia kelele, kamati iliyachukua na sasa yanakwenda kufanyiwa kazi, kwahiyo sisi kama chama tunapongeza," alisifu.

Kiongozi huyo wa MAT alisema kuwa kwa kuwa kamati ilitoa nafasi ya watu kupeleka maoni pale wanapoona kuna mahali pa kuboresha, wao kama chama wako tayari kufanya hivyo wakati wowote.

"Na bahati nzuri kamati ilisema kwamba milango iko wazi kwa wizara na mfuko wenyewe kwamba kama kuna maeneo tunafikiri bado tuna maoni na maboresho, tuyapeleke kiofisi, na sisi chama tuko tayari tutafanya hivyo.

"Kwahiyo, kwa ujumla tumeshiriki katika kuboresha hiki kitita ambacho kinakwenda kuanza kutumika hivi karibuni na tunaunga mkono kwa sababu kinakwenda kujibu sehemu ya malalamiko ya madaktari ambayo walikuwa wamesema, hasa wanaofanya kazi kwenye hospitali za mkoa kushuka chini," alisema.

Dk. Ndilanha alisema NHIF ni muhimu sana kwa nchi, hivyo ni muhimu kila mmoja kulinda mfuko huo kwa gharama yoyote ili usife.

"Mfuko wetu huu ni muhimu kwa nchi na huwezi kuzungumzia maboresho ya sekta ya afya bila kutaja NHIF na sisi sote tuna wajibu wa kuulinda ili usife kwa namna yoyote ile.

"Kama kutakuwa na changamoto yoyote ile, njia nzuri ni majadiliano na kufikia mwafaka ili wote twende kwa pamoja, ni mfuko wa kuigwa kwa Afrika," alisema.

HOSPITALI BINAFSI

Wakati kukiwa na hoja hizo za MAT, Chama cha Wenye Hospitali Binafsi (APHFTA) kimeendelea kukazia msimamo wake wa kutopokea wagonjwa wenye kadi za NHIF kuanzia leo.

Mwenyekiti wa chama hicho, Dk. Egina Makwabe alitoa tamko hilo jana baada ya kufanyika kikao jijini Dar es Salaam na kutoa azimio hilo.

"Kuanzia saa sita usiku leo (usiku wa kuamkia leo) hospitali binafsi tumeazimia hatupokea mgonjwa mpya mwenye kadi ya NHIF na walioko wodini wenye hali mbaya tutaendelea kuwahudumia ndani ya saa 48.

"Wagonjwa ambao watakuwa hawajapona ndani ya saa 48 tutafanya smooth transition ya kuwapeleka kwenye hospitali ambazo zitakubali kuwapokea wagonjwa hao."

MKURUGENZI NHIF

Katika mazungumzo na Kituo cha Redio cha Clouds FM cha jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benard Konga alisema kitita ni matakwa ya kisheria, kilianzishwa chini ya Sheria ya Bima ya Afya, Sura ya 395, ambamo mnatamkwa suala la kitita.

Alisema sura hiyo inaelekeza ni lazima yafanyike mapitio ya mara kwa mara, mara ya mwisho mapitio yalifanyika mwaka 2016.

Konga alisema kuwa kati ya mwaka 2016 na 2023, NHIF ilikuwa wanafanya mabadiliko madogo ili kuendana na uhalisia.

"Mwaka 2020 tulianza kufanya mapitio kwa kiwango kikubwa na Agosti Mosi, mwaka 2022 NHIF ilitoa taarifa kwa watoa huduma wote kwamba wameshatoa mapitio, wako tayari kutekeleza kitita kipya.

Alisema baada ya kutolewa taarifa hiyo, watoa huduma wengi walipinga wakisema hawajashirikishwa katika mchakato, wakaomba kushirikishwa.

"Serikali yetu ni sikivu, Waziri wa Afya aliagiza kuanzishwe machakato wa kuwashirikisha na  kuanzia Agosti 2022 tumekuwa na vikao vingi sana vya kujadili, kuboresha kitita.

"Ilipofika Desemba 2023 majadiliano yalimalizika na ilipofika Januari 2024, tukaanza kutekeleza, tukatoa matangazo kwa watoahuduma, lakini wakasema hawajaona majumuisho ya mwisho. Hivyo wanaomba kuyaona," alisema.

Aliongeza: "Waziri wa Afya akasitisha kuanza kwa kitita Januari Mosi, akaamua kuunda kamati huru ya  wataalaamu ambayo ilikuwa na kazi ya kupitia mchakato wote uliofanywa na NHIF kisha ije na ushauri. Kamati ikamaliza kisha ikaja na vigezo vya bei."

Konga alisema kumefanyika maboresho kwa kuwa kila siku kunaiobukia magonjwa mapya, pia namna ya kuyatambua, kuyatibu na kuyachunguza.

Akitolea mfano, Konga alisema kuwa mwaka 2016 hapakuwapo ugonjwa wa corona (COVID-19) lakini sasa ugonjwa huo upo, kitita nacho lazima kiwe na ugonjwa huo .

"Tunaangalia huduma zilizopo nchini, tangu mwaka 2016 hadi sasa kuna maboresho mengi sana, vituo vingi vimejengwa hadi ngazi ya chini, madaktari wameongezeka. Je, kitita chako kinawatambua hawa? Kinatambua vituo?" alisema.

Pia alisema gharama za utoaji huduma zinabadilika kila wakati, zinapanda na kushuka, kwamba hivi sasa kuna watoa huduma wa dawa wengi.

Alisema sababu nyingine ni kupunguza malalamiko na kuongeza kiwango cha huduma zinazotolewa pasipo kumwathiri mtoahuduma.

Kadhalika, Konga alisema kuwa kwa watoahuduma, NHIF wameangalia maeneo makubwa manne ikiwamo eneo ambako mwanachama wa NHIF anakwenda kupata huduma kuanzia zahanati hadi hospitali.

Alisema kitita cha mwaka 2016 kilikuwa kinamwangalia daktari bingwa wa macho aliyeko Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na daktari bingwa wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa Amana.

Alisema daktari wa Hospitali ya Amana alikuwa analipwa malipo kidogo kulinganisha na daktari wa MNH, ingawa wote wamesoma darasa moja na wanatoa huduma zinazofanana.

Alisema katika kitita kipya, NHIF wanamtambua madaktari kutoka ngazi ya chini kulinganisha na awali kuanzia ngazi ya wilaya.

"Na wao hivi sasa (madaktari wa chini) wataanza kulipwa kwa kiwango sawa na waliopo MNH, hii inaongeza morali na motisha ya kufanya kazi," alisema.

Konga alisema utoaji dawa ni eneo lingine ambalo linaingiza fedha nyingi kwa vituo vya kutolea huduma.

"Tulifanya mapitio, kuna dawa zaidi ya 200 ambazo hazikuwapo lakini tumeziongeza. Sasa tuna dawa kutoka 700 hadi 900, hii ni faida kubwa kwa mwanachana na mtoahuduma.

"Kuna dawa zaidi ya 200 bei zimeongezeka, yaani tulikuwa tunalipa bei ndogo. Kwa mfano, paracetamo tulikuwa tunalipa Sh. 20, sasa hivi tunakwenda kuziongezea bei," alisema.

Alibainisha kuwa kuna dawa ambazo walikuwa wanalipa bei kubwa (NHIF), sasa wanakwenda kuzishusha, zipo za aina 200, akisema hapo ndipo kuna malumbano kati yao na watoahuduma.

Mkurugenzi huyo pia alitaja eneo ambalo nalo wanakwenda kulifanyia mapitio, aina vipimo za 300 na operesheni, baadhi vinakwenda kushushwa bei.

*Imeandaliwa na Beatrice Shayo, Elizabeth Zaya na Joseph Mwendapole

Top Stories