Enzi mpya Vitambulisho vya Taifa usajili ulipokwenda kielektroniki

16May 2023
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Enzi mpya Vitambulisho vya Taifa usajili ulipokwenda kielektroniki

MSONGAMANO wa watu katika Ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) karibu saa nane, kuanzia saa 1:30 asubuhi, muda ambao hutumika kwa uzalishaji mali, umeifanya mamlaka hiyo kuboresha huduma zake kwa kujikita zaidi kujiendesha kidigitali.

Vitambulisho vya Taifa. PICHA: NIDA

 

Katika kuboresha huduma zake za utoaji wa vitambulisho vya taifa, mamlaka hiyo imeamua kutengeneza mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao (online registration), ili kuondokana na changamoto hiyo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano NIDA, Godfrey Tengeneza, anabainisha kwamba, tangu waanze huduma ya utoaji vitambulisho vilivyozalishwa ni 11,423,829 ambapo kati ya hivyo, vitambulisho 9,703,222 vimegawiwa kwa wananchi husika.

Anaweka wazi kwamba mfumo mpya wa usajili kidigitali lengo lake si kuongeza kasi ya uzalishaji wa

vitambulisho, isipokuwa unarahisisha mchakato wa usajili kwa kupunguza muda mrefu ambao mwananchi anautumia akienda kusajili katika ofisi za usajili wilayani.

Tengeneza anasema katika eneo la usajili na utambuzi wa watu, kumekuwa na ongezeko kubwa la wananchi wanaohitaji huduma hiyo.

“Hali hii inasababisha msongamano wa watu wengi katika ofisi zetu za usajili wilayani. Kwa kuzingatia hilo, tumeamua kutengeneza Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao yaani (Online Registration), ili mwombaji aweze kusajiliwa katika mfumo wa vitambulisho vya taifa, ni lazima afike katika Ofisi ya NIDA (wilaya) anayoishi kupata huduma.

Anaeleza kuwa  usajili wa taarifa za mwombaji katika mfumo wa usajili ulinasababisha foleni na usumbufu kwa waombaji kutokana na kukaa muda mrefu, kadhalika mamlaka inatumia gharama kuchapa fomu zinazotumika, kufanya manunuzi ya vifaa kwa ajili ya kupakia viambatanisho vya waombaji.

Pia anasema mamlaka inatumia gharama ya kusimamia mchakato wa usajili pamoja na uchakataji wa taarifa za waombaji. Hivyo, Tengeneza anasema mamlaka imejenga mfumo mpya wa usajili ili kumwezesha mwombaji kujisajili kwa njia ya mtandao na kukabiliana na changamoto hizo.

KUJISAJILI

Anaongeza kuwa usajili kielektroniki unalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma ya usajili wa raia pamoja na wageni na kwamba ili kujisajiliwa mtandaoni, mwombaji akishaingia katika mtandao wa internet ataandika eonline.nida.go.tz kisha atagonga mahali palipo andikwa jisajili na baada ya hapo, atajaza fomu kwa kufuata maelekezo na kwamba  mfumo unamwezesha mwombaji kujaza fomu akiwa  popote.

“Baada ya kujaza fomu hiyo, mwombaji anatakiwa kuchapa fomu na kuipeleka kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wake kwa ajili ya kugongewa mhuri na saini,”anafafanua na kusema  mwombaji anatakiwa kufika katika Ofisi ya NIDA iliyoko katika wilaya yake akiwa na fomu iliyokamilika iliyogongwa mhuri na kuwekwa saini ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, pamoja na nakala za viambatisho vyake alivyopakia katika mfumo wakati wa usajili ili kukamilisha taratibu za usajili (kuhojiwa na uhamiaji na kuchukuliwa alama za vidole ( biometria).

Anasema mfumo mpya wa usajili unampunguzia mtu changamoto mbalimbali zinazotokana na njia

inayotumika sasa katika usajili wa taarifa za mwombaji wa vitambulisho vya taifa, anataja faida zipatikanazo serikalini, NIDA pamoja na waombaji kupitia mfumo huo kuwa utatanua wigo wa usajili kwa kusogeza karibu huduma ya usajili kwa raia na wageni wakaazi kwa kuwa utapatikana kila mahali kwa kutumia kifaa chenye uwezo wa kupokea mtandao wa mawasiliano.

“Ujenzi wa mfumo mpya utapunguza gharama zinazotumika katika kuchapisha fomu za usajili na pia

kupunguza gharama za uchakataji wa taarifa. Kupunguza usumbufu kwa waombaji wa vitambulisho

vya taifa ambao wanafika ofisi za NIDA kwa ajili ya kuchukua fomu ya usajili na kujaza kwa ajili ya maombi ya kitambulisho cha Taifa; kwa kuwa zoezi la ujazaji wa fomu na kuambatanisha viambatisho litafanyika akiwa mahali popote,” anataja.

Faida nyingine anaitaja kuwa ni utapunguza muda unaotumika katika kusajili taarifa za mwombaji kwa

kuwa zoezi la kusajili taarifa zao litakuwa limefanywa na mwombaji mwenyewe. Anasema matarajio ya NIDA ni kwamba ujenzi wa mfumo huo mpya utaongeza idadi ya watu wanaohitaji huduma ya usajili kwa kuwa itapatikana mahali popote.

 

Top Stories