Kilichosikika Kariakoo ni sehemu ndogo ya vilio na malalamiko mengi ya jumuiya mbalimbali za Watanzania ambao wana kero nyingi wanazotamani kuzitoa. Mfano kuna wasafirishaji kuanzia daladala hadi malori ya shehena, hawa wanapoanza siku kila hatua wanayotembea ni mkono, unaotaka kitu kidogo.
Wapo wawekezaji binafsi kwenye huduma za afya maabara, zahanati na hospitali na pia wapo waliojitumbukiza kwenye elimu wakijenga shule za msingi, sekondari vyuo na vyuo vikuu wana vilio vyao ni kilio cha vikwazo, kodi, tozo na ada.
VIJIJINI WAPO
Baadhi ya watu wanaotamani kukutana na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa ni wakazi wa Kitongoji cha Kambulwa wakulima na wafugaji takribani 400, ambao wanaishi Kwamgome wilayani Handeni mkoani Tanga.
Wanacholia ni njaa, hawajalima masika wala vuli tangu mwaka jana baada ya ardhi yao kutwaliwa na serikali ili kuchimba kifusi, kokoto na mchanga kwa ajili ya ujenzi wa barabar a kutoka Handeni hadi Dodoma, ikipitia Manyara, Singida hadi Dodoma.
Wanapofika kwenye ofisi za Nipashe wanasema: “ Sisi wananchi wa Kwamgome ni wafugaji na wakulima tunaolima eneo la Kambulwa, lakini maeneo yetu yamechukuliwa na Halmashauri ya Mji – Handeni kwa ajili ya kambi ya ujenzi, machimbo ya mawe, kifusi na kokoto za ujenzi wa barabara za kitaifa.” Wanasema katika waraka wanaouwasilisha.
Waraka wao kwa Waziri Mkuu una malalamiko ya watu 22 wenye sahihi zao wakieleza kuwa Oktoba 16, 2022 walimwandikia Mkurugenzi wa Mji Handeni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mkuu wa Mkoa Tanga na mbunge wa Handeni Mjini kuhusu malipo ya maeneo yao.
Wanasema ni sehemu wanayoitegemea kwa kilimo, makazi na ufugaji, wakihoji wanalipwaje kwa kuwa hawana sehemu ya kuishi, kufuga na kulima kwa ajili ya kupata chakula na kwamba muda wa kilimo tayari umepita wa vuli na masika na tayari ni miaka miwili sasa.
Wanasema katika barua yao kwa Waziri Mkuu Majaliwa, aliyoambatanisha na majina 22 ya wakalalamikaji, ambayo Nipashe ina nakala yake.
Wanaongeza kuwa maeneo yao yalishapimwa kisheria na kufanyiwa tathmini ya ardhi na hati wanazo kama sheria hiyo inavyotaka na kwamba tathmini ilifanyika Juni 16, 2022 na sasa ni karibu mwaka umepita.
Wanasema kuanzia Novemba 2022 uongozi wa mkoa umewapa maelekezo ya kutafuta maeneo mengine wanunue na kwamba watalipwa. Hofu yao ni kwamba muda umeshapita, lakini leo hakuna majibu wala mawasiliano yoyote na serikali wakilalamika kuwa hawana sehemu za kuishi au makazi , malisho ya mifugo na kilimo na kuhoji wataishije?
Wanachotaka kwa Waziri Mkuu na serikali ni kujua msimamo wa serikali kuhusu malipo yao, wakihoji watalipwa lini? Wanashangaa kuona kampuni iko ‘saiti’ inachimba mawe, kifusi, kokoto na mchanga lakini hawajalipwa fidia inakuwaje?
Wanawageukia Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Mji Handeni mbona wako kimya bila kuwaeleza kuna tatizo gani? Watendaji wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Taifa na Mkoa kwa vile mradi huo umechukua makazi yao wangeongea nao lakini wote wamekaa kimya.
Katika barua ya malalamiko wakulima hao na wafugaji 22 wanasema kilichotokea kwa wafanyabiashara wa Kariakoo kitoe funzo viongozi wa serikali wahudumie na kujali wananchi hasa maskini ambao wanaoitegemea na kuiamini serikali kwa kila jambo.
UTETEZI WA VIONGOZI
Zafarani Madayi ni Meneja wa Mazingira na Jamii TANROADS Taifa, anapoulizwa kuhusu madai ya wakazi wa Kwamgome, kuwa kampuni ya ujenzi (jina tunalo) imeshaingia kazini bila kuwalipa wananchi ambao ardhi imechukuliwa, anasema sheria zikifuatwa hakutakuwa na kulalamika.
Utaratibu na sheria unaelekeza kuwa kabla ya mkandarasi kuingia kwenye eneo kuchukua kifusi au kuanza kazi ni lazima awasiliane na uongozi wa eneo na awatambue wamiliki , waonyeshe mipaka yao, uthamini ufanyike, walipwe kisheria na wakubali kutoa maeneo yao yachimbwe mawe, mchanga, kokoto na kabla ya kufanya hayo sheria hairuhusu.
Zafarani anasema wanacholipiwa ni fidia ya ardhi na mazao na kwamba kama hawajapata haki yao waende TANROADS Mkoa wa Tanga, maana ina taarifa zote za barabara miradi mkubwa kwa midogo. Anawashauri kumchagua mwakilishi siyo waende kundi la watu 400 na baadhi ya vitu wanavyotakiwa kwenda navyo ni barua ya Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa au Kijiji au viongozi wa kata kuwathibitisha.
“Hata hivyo, wafuatilie na kujiridhisha kwanza kufahamu iwapo ardhi ni mali yao au ya kijiji maana kama ni ya kijiji hawatafidiwa badala yake halmashauri inayohusika italipwa mrahaba.” Anasema Zafarani.
TANGA YAWASHANGAA
Ofisi ya Meneja wa TANROADS Tanga, inakiri kuwa ardhi ya kitongoji cha Kambulwa imechukuliwa kwa ajili ya kupata kokoto, mchanga, mawe na kifusi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kilometa takribani 430 kuanzia Handeni kipita mikoa ya Manyara-Singida na Dodoma.
Hata hivyo, inawashangaa mbona hawajafikisha malalamiko yao ofisini humo? Inawakaribisha kwa Meneja wa Mkoa, wasilalamike wafike TANROADS na watapata majibu ya maswali yao na kwamba tangu kutangazwa hatua za kuchukuliwa eneo hilo hawajawasilisha malalamiko ofisi ya mkoa huo, anasema Meneja wa Mkoa, Eliazary Rweikiza.
Anawatoa hofu kuwa wamehamishwa eneo hilo, ili kuwalinda wasije kuumizwa na milipuko ya mawe na kwamba ni jambo linalofahamika hivyo wafike ofisi ya mkoa na watapatiwa majibu ya maswali yao anasema Rweikiza.




.jpeg?itok=vCj6bCRe)






