JKT Tanzania yataka ya JKT Queens

08Aug 2023
DAR ES SALAAM
Nipashe
JKT Tanzania yataka ya JKT Queens

KLABU ya JKT Tanzania ambayo imerejea tena Ligi Kuu, imesema lengo lao kwenye Ligi ya msimu wa 2023/24 ni kuzisaka nafasi nne za juu lengo likiwa ni kucheza michuano ya kimataifa na si kupigania ili isishuke daraja kama ilivyokuwa ikifanya huko nyuma kabla haijashuka.

 

Akizungumza juzi baada ya ushishi wa bao 1-0 dhidi ya Stand United ambayo nayo inajiandaa na Ligi ya Championship baada ya kupanda kutoka 'First League', Kocha Msaidizi wa timu hiyo, George Mketo, alisema wanatambua msimu ujao utakuwa mgumu, lakini na wao wamejizatiti kwa kufanya usajili bora ambao utawafanya kupigania nafasi nne za juu ili kusaka tiketi ya kucheza kimataifa kama ambavyo timu yao ya Wanawake, JKT Queens imefanya msimu uliomalizika kwa kutwaa ubingwa na itacheza michuano ya CECAFA kusaka nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.

JKT Tanzania iliyopiga kambi Shinyanga kwa ajili ya 'pre season', ilicheza mechi hiyo kwenye Uwanja wa Kambarage dhidi ya Stand United yenye maskani yake mjini humo.

"Tumeshacheza mechi tatu hapa, ya kwanza tumetoka sare na Kagera Sugar bao 1-1, ilikuwa ngumu na nzito, tumecheza na Kombaini ya Shinyanga, tumetoka sare ya mabao 2-2 na leo (juzi) tumecheza na Stand United tumepata ushindi wa bao 1-0, sisi kwetu matokeo si muhimu sana kwa sasa, ila tunaangalia jinsi gani wachezaji wetu wanafanya kile ambacho tumewaelekeza na kama wanakifanya kwa usahihi," alisema Mketo.

Hata hivyo, zipo taarifa kuwa huenda timu hiyo ikaweka makazi yake hapo na kucheza mechi zake za Ligi Kuu Uwanja wa Kambarage Shinyanga.

"Tumesajili wachezaji chipukizi na wazoefu na tunaamini mchanganyiko huo utatimiza malengo ya klabu ambayo kwa msimu ujao, si ile JKT Tanzania ya kucheza ili kubaki kwenye ligi haipo tena, tunazitaka zile nafasi nne za juu ambazo zitatupa nafasi ya kucheza kimataifa, hayo ndiyo malengo ya kwanza kabisa ya klabu yetu msimu ujao," alisema Mketo.

 

 

 

Top Stories