Kwanza naanza na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuhusu utendaji wa kazi zake. Sidhani kama linafanya kazi zake kwa weledi unaotakiwa au angalau kuiga mambo yanayofanywa na vyama vingine vya soka Afrika.
Wanaogombea nafasi za uongozi kwenye shirikisho hilo hugombea ili kuendeleza soka letu au ni kujitafutia ulaji tu? Sioni mpango wowote unaofanywa na viongozi wake ili kuzikwamua timu zetu za kandanda na kuipeleka nchi kwenye viwango vya juu vya kimataifa.
Nasema hivyo kwa sababu sasa Tanzania inashika nafasi ya 140 katika viwango vya Shirikisho la Soka Duniani, FIFA. Katika nchi za Afrika Mashariki, Uganda ndio inayoongoza kwa kuwa katika nafasi ya 82 ikifuatiwa na Kenya katika nafasi ya 112 huku Rwanda ikiwa nafasi 136.
Rwanda ni nchi ndogo sana ikilinganishwa na Tanzania kwani yaweza kuwa kama moja ya mikoa yetu. Pamoja na udogo wake ina wachezaji wazuri kuliko Tanzania!
Juu ya udogo wake, kama ilivyo pia Burundi, timu mbalimbali za Tanzania zina wachezaji na makocha kutoka nchi hizo! Pia kuna wachezaji kadhaa wa Rwanda na Burundi wanaocheza kandanda la kulipwa Kenya, Uganda na kwingineko.
Badala ya TFF kutafuta njia sahihi ya kuwaendeleza wachezaji wetu ambao naamini wapo wengi wenye viwango vizuri, eti imeongeza idadi ya wachezaji wa kigeni mpaka 10! Sasa Tanzania imekuwa kimbilio la wachezaji wa kigeni, wengi wao wakiwa na viwango vya chini kuliko wachezaji wetu.
Kama wachezaji wa kigeni ni hodari, mbona hawakimbilii kwenye nchi zenye vilabu vinavyojiendesha vyenyewe? Wanakimbilia Tanzania kwa sababu wanajua ndio nchi watakayojipatia fedha kirahisi. Tumekuwa ‘wajinga ndio waliwao!’TFF pia ilitoa tangazo kuwa msimu ujao wa Ligi Kuu utaanza bila kuwa na wadhamini baada ya Vodacom waliokuwa wadhamini kwa muda mrefu kuonesha dalili ya kutoendeleza udhamini wao kwa timu za Ligi Kuu.
Zipo tetesi kuwa huenda Vodacom ikaendeleza udhamini wake, lakini kama haikuwa hivyo, timu za Ligi Kuu zitakuwa katika hali tete. Vilabu vitapata wapi fedha za kusajili wachezaji wazuri na wakati huohuo kulipa mishahara yao na makocha?
Wanachama wanapaswa kuchagua viongozi wenye uwezo watakaoleta maendeleo na kufanya vilabu vijitegemee badala ya kuwategemea matajiri wanaoweza kuondoka wakati wowote.
Tazama hali ilivyokuwa kwenye klabu ya Simba kabla haijatwaliwa na MO Dewji mwenye asilimia 49 ya hisa. Hali hiyo sasa imeangukia Yanga inayohitaji mwekezaji mwenye uwezo wa kuitoa hapo ilipo kwa kuomba michango!
Sasa kuna kiongozi anayeng’ang’aniwa na wanachama ingawa aliandika barua ya kujiuzulu. Wanachama hawakumbuki alivyohadharisha kuwa wasimtegemee sana kwani yeye ni mwanadamu huenda asiwepo na kuwataka wajitahidi kuendesha klabu?
Jambo lingine linahusu makocha wa vilabu vyetu vya kandanda. Imekuwa kawaida vilabu kubadilisha makocha kama watanashati (watu wanaovutia kwa umaridadi wao, watu nadhifu) wafanyavyo kwa mavazi yao. Viongozi na wanachama wao hutaka mafanikio ya haraka.
Kocha anapopewa timu mpya, hukuta wachezaji wanacheza tofauti na mfumo wake. Hivyo anapaswa kupewa muda wa kutosha ili wachezaji wazoee mfumo anaotaka yeye. Katika hali kama hiyo si rahisi wachezaji kufuata mfumo wake haraka kama idhaniwavyo. Itokeapo timu kufanya vibaya, mara kocha anatimuliwa kuwa hafai!
Lazima kocha apewe muda wa kutosha ili mfumo wake uzoelewe na wachezaji anaowafundisha. Ndio maana baadhi ya makocha hubadili hata nafasi za wachezaji. Utaona mchezaji wa pembeni kuletwa kati, wa kati kwenda pembeni na hata mshambuliaji kurudishwa katikati n.k. kwa jinsi kocha mpya aonavyo inafaa.
Tuwape makocha nafasi ya kutosha kufanya kazi zao. Tusiwaingilie kama tulivyozoea. Kama kuna anayejua, basi ajitokeze na kuonesha mfano badala ya kukalia majungu na kuwalaumu makocha na wachezaji.
0715/0784 334 096