Tathmini iliyofanywa na Lete RAHA inaonyesha kuwa beki wa kulia wa Azam, Shomari Kapombe, ndiye mchezaji aliyefanya vizuri katika nafasi yake huku pia akitisha katika ufungaji kama straika.
Makipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ na Mustafa Ali ‘Barthez’, ndiyo makipa waliofanya vizuri zaidi wakiruhusu magoli machache zaidi ya makipa wengine kwenye ligi. Hamisi Kiiza wa Simba ameonesha uwezo mkubwa wa ufungaji akiwa na klabu yake ya Simba huku mabao yake yakichangia kwa kiasi kikubwa ushindi wa timu hiyo. Straika wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma na winga wa Mtibwa, Shiza Kichuya ndiyo chipukizi waliozibeba klabu zao.
Wafuatao ni baadhi ya nyota waliong’ara kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kwa msimu huu.
Shomari Kapombe (Azam)
Beki wa Azam, Kapombe ameweka rekodi ya kipekee ambayo haijashuhudiwa kwa muda mrefu kwenye Ligi Kuu. Kufikia sasa amefunga jumla ya mabao saba kwenye mechi 15 za ligi na kuwafunika mastraika wengi wa Ligi Kuu huku akilingana kwa mabao na mastraika wa timu yake ya Azam, John Bocco na Kipre Tcheche ambapo kila mmoja ana mabao saba.
Kapombe amekuwa kati ya mabeki wa pembeni wanaofanya vizuri msimu huu. Amekuwa na nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha timu yake. Wachambuzi mbalimbali wa soka nchini wanadai kuwa beki huyo yuko kwenye kiwango cha juu ambacho hajawahi kuwa nacho hapo awali tangu alipokuwa akiitumikia klabu ya Simba. Anaweza akawa ndiye mchezaji bora wa mzunguko wa kwanza.
Michael Aidan (JKT Ruvu)
Nahodha wa JKT Ruvu, Michael Aidan naye amekuwa akifuata nyayo za Kapombe na kwenye klabu yake, ndiye mchezaji anayefanya vizuri akifunga mabao na kutengenezea wenzake mabao. Amekuwa akipamba na alichangia zaidi kwenye ushindi mkubwa wa timu yake wa 4-1 dhidi ya Prisons kwa mwaka jana. Beki huyo mwenye kasi na uwezo mkubwa wa kukaba alifunga mabao mawili kati ya manne ya timu hiyo. Uwezo wake ni dhahiri kuwa ni miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri msimu huu. Kwa Ruvu, straika Samuel Kamuntu pia ni kati ya wachezaji waliotamba na kuisaidia timu hiyo inayonolewa na kocha Abdallah Kibadeni.
Jeremiah Juma (Prisons)
Hakuna ubishi, huyu ndiye straika anayekuja kwa kasi ya juu kwenye ligi kwa msimu huu, Jeremiah Juma wa Prisons amefanikiwa kufunga jumla ya mabao tisa kwenye ligi mpaka sasa akiwa karibu kuwafikia Amissi Tambwe na Hamisi Kiiza wanaoongoza.
Straika huyo ni mchezaji wa kipekee na mwenye uwezo wa tofauti na mastraika wengine Prisons. Ni mzuri kwenye kukokota mpira, kufunga mabao na kukaba. Jeremiah anajiamini na ndiye mchezaji aliyechangia zaidi mafanikio ya Prisons kwenye mzunguko wa kwanza uliomalizika hivi karibuni. Kwenye kikosi cha Prisons, straika Mohamed Mkopi naye amekuwa akipambana na kufunga mabao.
Kelvin Yondani (Yanga)
Beki Kelvin Yondani wa Yanga kwa msimu huu amekuwa na nidhamu ya tofauti na amekuwa na kiwango chake huku akiisadia Yanga wakati Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Vincent Bossou walipokuwa wakipishana kwenye nafasi ya kucheza pembeni ya Yondani.
Yondani aliendana vyema na Bossou, lakini pia aliendana na Cannavaro na licha ya kuwapo kwa mabadiliko kwenye safu ya ulinzi, beki huyo ameisaidia Yanga kwenye mechi 15 zilizopita. Utulivu na umakini wake uliisaidia Yanga.
Hamisi Kiiza (Simba)
Straika wa Simba, Amissi Kiiza amekuwa na msimu mzuri mpaka sasa akiwa tayari amefunga mabao 10 kwenye mechi 12 alizoichezea klabu yake kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi. Mwanzoni mwa msimu huu straika huyo alikosa mechi tatu baada ya kuumia goti na aliporejea alirudi na makali yake na kwenye mchezo miwili ya mwisho amefunga mabao mawili na kuibeba Simba. Kiiza anatajwa kuwa miongoni mwa mastraika watakaoweza kutwaa tuzo ya kiatu cha cha dhahabu ya mfungaji bora mwishoni mwa msimu huku akipambana na Amissi Tambwe ambaye hakamatiki kirahisi.
Amissi Tambwe (Yanga)
Ni mwaka mmoja sasa tangu straika huyo alipojiunga na Yanga akitokea Simba. Tambwe alijiunga na Yanga kipindi cha dirisha dogo alipotemwa na Simba, lakini sasa amekuja kuonyesha bado yuko juu na ndiyo maana alishika nafasi ya pili kwa ufungaji wa mabao msimu uliopita. Msimu huu pia anaongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi akiwa tayari amefunga mabao 13 katika mechi 15 za mzunguko wa kwanza.
Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar)
Winga huyu amewabwaga mastaa kama Deus Kaseke wa Yanga, Farid Mussa wa Azam, na kikubwa ni kuwa Kichuya ni winga mwenye umbo dogo, lakini mwenye uwezo wa juu anapokutana na mabeki wenye miili mikubwa. Kichuya ni mbunifu na mwenye uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira. Ana kasi na mwenye uwezo wa kutengenezea wenzake mabao. Ameifungia Mtibwa mabao matatu kwa msimu huu, lakini pia amepika mabao sita. Kichuya ameibuka kuwa moja ya wachezaji tishio kwa timu pinzani.
Salim Gilla (JKT Mgambo)
Salim Gilla ni straika mpambanaji wa JKT Mgambo ambaye ni mjanja wa kutumia uzembe wa mabeki wa timu pinzani. Gilla amecheza mechi minne na kufunga mabao matatu. Walipofungwa bao 4-1 dhidi ya JKT Ruvu, yeye ndiye aliyepiga la kufutia machozi. Pia alifunga kwenye sare ya 1-1 dhidi ya Mbeya City na pia akafunga walipopoteza kwa bao 2-1 dhidi ya Azam.
Atupele Green (Ndanda)
Ni moja kati ya washambuliaji mahiri kwenye ligi kwa msimu huu. Atupele amekuwa ni mshambuliaji aliyeiwezesha Ndanda kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja kwa kuipandisha hadi kwenye nafasi ya 11 kwenye ligi yenye timu 16.
Alichangia zaidi kwenye ushindi mkubwa wa 4-1 walioupata Ndanda dhidi ya Mbeya City Jumatano. Atupele ni kati ya wachezaji ambao wamekuwa wakifanya vizuri licha ya kuwapo kwenye timu ambazo zimekuwa zikikosa mwelekeo mzuri kwenye Ligi. Ana uwezo binafsi lakini pia anaweza kuiunganisha timu yake.
Deogratius Munishi ‘Dida’ (Yanga)
Kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ni kati ya makipa waliofanikiwa kufanya vizuri zaidi kwa msimu huu akipokezana na kipa Mustafa Ali ‘Barthez’. Makipa hao waligawana mzunguko wa kwanza, mmoja akicheza mechi saba na mwingine nane na waliibuka kidedea kwa kuweka rekodi ya kutofungwa mabao mengi wakiruhusu magoli matano tu katika mechi 15 za mzunguko wa kwanza wakati makipa wa Azam na Simba wameruhusu mabao tisa kila timu. Dida tangu alipofungwa magoli mawili katika sare ya 2-2 dhidi ya Mwadui mjini Shinyanga Oktoba 28, mwaka jana, hajaruhusu bao katika mechi saba mfululizo.




.jpeg?itok=vCj6bCRe)






