Alianza kwa kumteua Waziri Mkuu ambaye ni Kassim Majaliwa, akathibitishwa na wabunge kama hitaji la kikatiba na kisha akateua mawaziri wake mwezi uliopita.
Uteuzi wa Baraza la Mawaziri ulipokelewa kwa hisia tofauti, huku wengi wakipongeza na baadhi wakiponda na hususan madai kwamba kuna baadhi ya mawaziri walioonekana mizigo katika serikali ya Awamu ya Nne aliwateua tena.
Watu pia wamekuwa wakijiuliza imekuwaje amechukua mawaziri wengi nje ya wabunge wa chama chake, CCM, ambao ni zaidi ya 200.
Lakini kabla sijafika mbali, ni vyema niweke maelezo haya muhimu kwamba tunaposema waziri, tunamaanisha kiongozi mwandamizi katika nchi yetu, ambaye wananchi tunajinyima (kwa kuruhusu kodi zetu kutumika kwa ajili yake) ili kumpa ofisi yenye hadhi kubwa, mshahara mnono, usafiri na marupurupu mengine lukuki ili kutufanyia kazi wananchi.
Kwa hiyo Waziri ni mtumishi muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu na ambaye utumishi wake kwa umma unatakiwa kuakisi hayo ambayo wananchi wanajinyima kwa ajili yake.
Nianze kwa kusema kwamba kwa kiasi kikubwa, Rais John Magufuli amejitahidi kuja na baraza ambalo mimi binafsi silitilii mashaka sana kwa maana ya kwamba sura nyingi zilizomo zinaonesha kwamba zinaweza kutufanyia kazi tunayoitarajia, mintarafu suala zima la maendeleo ya nchi yetu.
Lakini pengine baraza lake lingeweza kuwa zuri zaidi kama Katiba ya wananchi, kwa maana ya ile iliyokuwa imependekezwa na Tume ya Jaji Warioba, ingepita kama ilivyokuwa imependekezwa kabla ya 'kuchakachuliwa' na Bunge la Katiba.
Kwanza kama katiba ingelipita kama ilivyokuwa imeombwa na wananchi na tukaingia kwenye uchaguzi mkuu uliopita na katiba hiyo, hii maana yake ni kwamba, hata kama kipengele cha wabunge kutokuwa mawaziri kisingepita, Magufuli angepata mawaziri wengi wazuri kutoka kwa wabunge waliochaguliwa na CCM bila kulazimika kusaka nje.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba katiba ya Warioba ilijikita katika kutupatia wananchi wabunge waadilifu na wawajibikaji kwani iliwataka wananchi kuwa na uwezo wa kumuondoa madarakani mbunge ambaye anashindwa kutimiza wajibu wake na pia kuweka ukomo wa maisha ya mbunge.
Hii maana yake ni kwamba baadhi ya wabunge, ambao kwa bahati mbaya wengi wako chama tawala, wasingeligombea kutokana na kujijua kwamba si waadilifu na wawajibikaji isipokuwa wanapata ubunge kutokana na fedha zao na kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
Hatua ya Magufuli kulazimika kuteua mawaziri wengi nje ya wabunge wa chama chake na pia kukaa muda mrefu bila kupata wengine wanne, ili kujaza nafasi zilizokuwa wazi inadhihirisha udhaifu huo.
Ninataka kusema kwamba kama tungekuwa na utawala mseto ambapo rais anaruhusiwa kuchagua waziri kutoka chama chochote, angelipata wengi kutoka upinzani. Nina hakika watu kama Zitto Kabwe, John Mnyika, Ester Bulaya, Abdallah Mtolea (mbunge wa Temeke kupitia CUF) na wengine lukuki wangeliweza kushika ofisi hizo kubwa za umma na kuwatumikia Watanzania kukidhi mahitaji yao.
Lakini kama katiba ya Warioba ingelipita kama ilivyokuwa kwamba mawaziri wasiwe wabunge, hapo napo Rais Magufuli angelikuwa na uwanja mpana sana katika uteuzi wake kwani huku nje ya mwaziri kuna watu wengi wazuri lakini hawana mpango wa kugombea ubunge kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na chaguzi za siku hizi kutawaliwa na uwezo wa kifedha na siyo uwezo wa kuwatumikia wananchi aliyo nao mtu.
Lakini kubwa kabisa ambalo nilitaka kulizungumzia katika makala haya ni kwamba, Baraza la Mawaziri lingekuwa zuri zaidi kama kungekuwa na chombo kingine kinachoidhinisha uteuzi wa mawaziri alioufanya rais.
Unapokuwa na katiba kama hii yetu ambayo rais ameachiwa kuteua yeyote amtakaye, alimradi awe mbunge [kwa kuchaguliwa, viti maalum ama yeye mwenyewe kumteua ubunge] huwezi kukosa mawaziri ambao wanapewa nafasi hiyo muhimu kwa sababu mbali mbali kama vile udugu, urafiki, kulipa fadhila na kadhalika.
Bila kutumia mifano ya hapa nyumbani lakini hili lilijitokeza kwa hayati Rais Michael Sata wa Zambia baada ya kuchaguliwa na kuingia madarakani mwaka 2011. Pamoja na kujipambanua kama mtu anayepinga sana ufisadi, pamoja na kujitahidi kufanya mambo mengi ambayo yaliwafurahisha sana Wazambia kwa kuwaondolea kero mbalimbali ambazo zilikuwa zimeshindikana kuondolewa na watawala waliokuwa wametangulia lakini kwa vile katiba ilikuwa kama hii yetu alitumbukia kule kule; kuteua mawaziri kwa njia ya udugu, urafiki ama kulipa fadhila.
Hata ambaye aliwahi kuwa waziri katika serikali ya Hayati Frederick Chiluba kupitia chama cha Multiparty Democracy, alilalamikiwa kwa kumteua mjomba wake, Alexander Chikwanda, kuwa waziri wa fedha pamoja na mpwa wake, Miles Sampa, kuwa makamu waziri wa fedha. Mwingine alikuwa ni Waziri wa serikali za mitaa aliyekuwa balozi wa nchi hiyo nchini Japan.
Ukija hapo kwa majirani zetu Uganda ndio kabisa. Rais Yoweri Museveni ana mlolongo mkubwa wa ndugu zake katika madaraka makubwa ya kuongoza serikali akiwamo mkewe.
Sisemi kwamba kuna mawaziri ambao Rais Magufuli amewapa nafasi hiyo kutokana na sababu za uswahiba, udugu au kulipana fadhila, lakini imani yangu ni kwamba kama wangelikuwa wateule wake wanalazimika kuthibitishwa na Bunge kwanza kwa kura ya siri, angelikuwa makini zaidi katika uteuzi wake kuliko ilivyo sasa.
Tujue kwamba umimi ndio ubinadamu wenyewe. Tabia ya binadamu wengi tulivyo ni ngumu sana kuuzuia umimi na inasemekana kwamba pamoja na uzalendo aliokuwa nao Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuna maeneo ambapo aliteua watendaji wa serikali yake kutokana na udugu na wengine wanakwenda mbali na kutaja udini ingawa pia si rahisi kuthibitisha madai haya.
Ingawa udugu, urafiki ama ukaribu wowote si kigezo cha mtu kutopewa madaraka kama ana uwezo, lakini huko nyuma tumeshuhudia kuona ndugu au marafiki wakipewa madaraka makubwa siyo kwa sababu ya uwezo wao ama hakuna wananchi wengine ambao wangeweza kufanya kazi hiyo hiyo kwa mafanikio makubwa isipokuwa kutokana na ‘umimi’ tu alio nao mwenye mamlaka ya kuteua.
Haya, sasa tunao mawaziri ambao mimi ninaamini wamo maswahiba wa Rais (kwa sababu ndio ubinadamu wenyewe). Je, watakapofanya madudu ni kweli atachukua maamuzi ya kuwandoa mara moja? Na asipochukua maamuzi magumu ya kuwabadili nini kitafanyika? Ndio maana tunahitaji katiba itatakayoangalia pia maeneo hayo.
Mwalimu Nyerere alipata kusema kwamba, katiba hii ya mwaka 1977, inampa madaraka makubwa sana rais na kwamba kama atayatumia anavyotaka anaweza kuwa dikteta. Mwalimu alilenga eneo ambalo Rais kwa katiba hii ndiye anayeteua karibu kila mtu. Kwa hiyo inabaki kuwa katiba ya kuomba mpate rais ambaye hatotumia madaraka yake ya uteuzi wa kila kiongozi vibaya. Na mbaya zaidi, wateule wengi wa rais wakiwamo wakuu wa mikoa na wilaya, humfikiria au kumtumikia zaidi aliyewateua kuliko wananchi anaodaiwa kuwatumikia!
Ndipo swali linakuja. Je, tutaendelea kuwa na katiba kama hii hadi lini?
Ndio maana inatakiwa sasa tuanze kudai katiba mpya na mimi ninashauri tuanzie pale alipofikia Warioba na Tume yake na hivyo liundwe bunge lingine la katiba litakaloboresha katiba hiyo.
Katiba ingeliweza kutupa Baraza zuri zaidi la Mawaziri
17Jan 2016
Taifa Letu
Katiba ingeliweza kutupa Baraza zuri zaidi la Mawaziri
BAADA ya kuonekana kama amechelewa ukilinganisha na watangulizi wake, hatimaye Rais John Magufuli, aliweka hadharani baraza lake la mawaziri ambalo lilikuwa likisubiriwa kwa muda mrefu na wananchi.
Jaji Joseph Wariona




.jpeg?itok=vCj6bCRe)






