Leo nitajadili hali ilivyo katika nchi jirani ya Rwanda ambayo pia ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), baada ya Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame, naye kutaka katiba ya Rwanda ibadilishwe ili aendelee kuwapo madarakani licha ya kuiongoza nchi hiyo toka mwaka 2000.
Kabla ya kujadili hatua ya Kagame ya kutaka kudumu madarakani kwa miaka 17 ijayo, nimalizie hali ya Burundi ambayo inaendelea kuwa tata kila uchao kutokana na Rais Nkurunzinza na serikali yake kuedelea kupuuza wito wa Jumuiya ya kimataifa wa kupelekwa kwa vikosi vya kulinda amani nchini humo kwa ajili ya kuwalinda raia dhidi ya mauaji yanayoendelea kutokea kila siku katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bujumbura.
Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Katibu Mkuu, Ban Ki Moon, umeshaidhinisha kupelekwa kwa wanajeshi 5,000 nchini Burundi kwa ajili ya kulinda mamia ya watu ambao watatoka katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).
Rais Nkurunzinza na serikali yake wanapinga mpango huo wakidai kuwa serikali ya Burundi inao wajibu na uwezo wa kuwalinda raia wake. Hakuna sababu ya kulindwa!
Serikali hiyo inasema kuwa kuna usalama wa kutosha nchini humo na kwamba hakuna sababu za kupelekwa kwa wanajeshi wa kulinda amani nchini huyo. Inaendelea kudai kuwa ndiyo maana Burundi imechangia vikosi vya kulinda amani katika nchi mbalimbali duniani zinazokabiliwa na migogoro ikiwamo Somalia.
Hata hivyo, wakati Nkurunzinza na wenzake wakiendelea na msimamo wa kutokutaka kupelekwa kwa vikosi vya kulinda amani, maelfu ya raia wa nchi hiyo inaripotiwa kuwa wanaendelea kukimbilia katika maeneo mengine ya nchi hiyo na wengine kuvuka mipaka kwenda kuishi maisha ya ukimbizi katika kambi za wakimbizi zilizoko nchi jirani za Rwanda, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kama nilivyoeleza katika makala yangu ya wiki iliyopita, upatanishi wa mgogoro huo bado unasuasua kutokana na mpatanishi wa sasa, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, kuonyesha kuwa ameshindwa kuzipatanisha pande zinazohusika.
Hali hiyo ilidhihirika jijini Entebbe baada ya kukwama kwa mazungumzo yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Januari 6, mwaka huu, kufuatia hatua ya wahusika kueleza kuwa hawakuwa tayari kuendelea na mazungumzo hayo.
Hata hivyo, wiki iliyopita, Tanzania ambayo ni mwenyekiti wa EAC kupitia kwa Waziri wake wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, ilisema kuwa jitihada za upatanishi wa Burundi zinaendelea na kwamba kuna kamati iliyokutana ikizihusisha baadhi ya nchi ikiwamo Tanzania na Angola kuangalia namna ya kuandaa mkutano wa kuzikutanisha pande husika.
Balozi Mahiga alisema kuwa kinachoshughulikiwa kwa sasa ni kuangalia ni makundi gani yaalikwe katika mazungumzo yajayo huku akiendelea kumtaja Rais Museveni kuwa ndiye mpatanishi.
Kwa hali ilivyo sasa Museveni hawezi kuwa msuluhishi wa maana katika mgogoro huo kwa kuwa kinacholalamikiwa Burundi cha Nkurunzinza kutaka kubakia madarakani ndicho anachokifanya yeye nchini humo, hivyo, hawezi kumnyooshea kidole nkurunzinza na wenzake.
Mwanazuoni nguri wa siasa na mahusiano ya kimataifa ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Profesa Mwesiga Baregu, anasema kuwa Museveni ameshindwa kabisa kusuluhisha mgogoro wa Burundi na kuwakosoa viongozi wa EAC kwa kutoteua msuluhishi mwingine. Profesa Baregu anakwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa kwa kuwa Tanzania ndiye mwenyekiti wa EAC, basi inapaswa kuchukua nafasi yake ya kuusuluhisha mgogoro huo.
Binafsi ninamshauri Rais John Magufuli kama mwenyekiti wa EAC ateue mtu mzoefu na anayekubalika nchini Burundi kuzipatanisha pande zinazohusika. Kwa kuwa Tanzania ina ushawishi mkubwa nchini Burundi, sio vibaya akawateua baadhi ya viongozi wetu wastaafu kama Benjamin Mkapa, Joseph warioba au Dk. Salim Ahmed Salim kuwa msuluhishi wa mgogoro wa Burundi.
Nikirudi katika mada yangu ya leo kuhusu Rwanda, ni kwamba hatua ya Rais Kagame ya kuitisha kura ya maoni ya kuamua kubadilisha katiba ya nchi hiyo ili kumuongezea muda wa kubaki madarakani, inaleta doa lingine katika EAC.
Nchi wanachama wa jumuiya hiyo zimekuwa zinatekeleza hatua mbalimbali za kushirikiana kuelekea shirikisho la kisiasa, lakini kitendo cha baadhi ya nchi kutokuwa tayari kuweka ukomo wa muda wa madaraka ya marais kitakwamisha jitihada hizo kwa kuwa bila demokrasia na utawala bora haiwezekani kuwapo shirikisho la kisiasa.
Katika kura ya maoni iliyofanyika Rwanda, Asilimia 98.4 ya wananchi walikubali kufanyika kwa marekebisho ya katiba kuongeza vipindi vya urais hatua inayompa Rais kagame miaka 17 zaidi na kumwezesha kuendelea kuwa madarakani hadi mwaka 2034.
Pamoja na kwamba Rais kagame aliingia madarakani rasmi mwaka 2000, lakini kiuhalisia ndiye aliyekuwa kwenye udhibiti wa Rwanda tangu mwaka 1994, baada ya vikosi vyake vya waasi wa Rwandese Patriotic Front (RPF) kutoka msituni na kudhibiti mauaji ya kimbari yaliyoikumba nchi hiyo.
Aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Pasterius Bizimungu, alikuwa rais boya tu, lakini udhibiti wote wa dola na jeshi alikuwa nao Kagame huku akijiita Makamu wa Rais. Ndiyo maana baadaye Kagame alimuondoa madarakani Bizimungu, kuamuru akamatwe na kufungwa jela.
Hatua hiyo ya Kagame ya kutaka kubadili katiba ili aendelee kuwa madarakani imekosolewa na baadhi ya mataifa ikiwamo marekani na wanyarwanda kadhaa hususan wanaoishi uhamishoni, wakisema kuwa amefanya hivyo kwa maslahi yake binafsi.
Wanaomkosoa Kagame wanasema kuwa hata kama kuna waliopiga kura ya hapana haikuwa rahisi kubadili matokeo ya kumpinga kwa sababu amedhibiti kila kitu.
Jumuiya ya Afrika Mashariki haikua salama kutokana viongozi wa nchi wanachama zikiwamo Burundi, Rwanda na Uganda kutokuwa tayari kuweka ukomo wa uongozi wa marais na hilo litaendelea kuzitesa nchi hizo na kutishia utulivu wake. Unaweza kusema kwamba Rais Kagame naye amefuata njia ile ile ya Rais Nkurunzinza, ambayo inawasababishia mateso na mahangaiko makubwa wananchi wa Burundi kwa sasa.
Ni jambo lisilo na ubishi kwamba Rais Kagame ameleta utulivu licha ya kulalamikiwa kuminya uhuru wa vyombo vya habari na vyama vya siasa kutokana na kitendo chake cha kudhibiti mauaji ya kimbari nchini humo yaliyosababisha vifo vya takribani watu milioni moja pamoja na kujenga umoja wa kitaifa nchini huo.
Hata hivyo, inatosha sasa kwa Rais Kagame kuweka mazingira ya kustaafu na kuwaachia watu wengine kuiendeleza nchi hiyo katika misingi hiyo hiyo. Na kwa kufanya hivyo, Wanyarwanda na dunia watamkumbuka.