Deschamps: Benzema atakuwa fiti Kombe la Dunia

12Nov 2022
Na Mwandishi Wetu
PARIS UFARANSA
Nipashe
Deschamps: Benzema atakuwa fiti Kombe la Dunia

KOCHA wa Ufaransa, Didier Deschamps amedai kuwa Karim Benzema 'analipa gharama’ kwa kucheza sana miaka ya hivi karibuni baada ya kusumbuliwa na majeraha hadi sasa msimu huu, lakini ana imani fowadi huyo wa Real Madrid atakuwa fiti kwa wakati kwa mechi ya kwanza ya Les Bleus hao kwenye Kombe la Dunia

Benzema hakuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichonyanyua taji la Kombe la Dunia 2018 kwa sababu ya kutoshiriki kwa muda mrefu katika majukumu ya kimataifa baada ya kashfa yake ya kuvujisha mkanda wa video ya ngono ya mchezaji mwenzake mwaka 2015.

Lakini aliitwa tena na Deschamps kwenye Euro 2020 mwaka jana, kabla ya kuwa na msimu bora zaidi wa maisha yake yote akiwa na Real, akishinda LaLiga, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ballon d'Or.

Benzema amefunga takribani bao moja kwa kila mechi kwenye LaLiga msimu huu, lakini matatizo ya misuli na uchovu vimemfanya afikishe mechi saba pekee za nyumbani, huku akiwa hajafunga kabisa katika mechi nne za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa Los Blancos hao.

"Anajua kuwa Kombe la Dunia ni wakati muhimu sana kwake. Atafanya kila kitu, kama kundi zima, kuwa tayari Novemba 22,” alisema Deschamps akiiambia TF1.

“Kuna kipindi Benzema alicheza sana na sasa analipa gharama kutokana na majeraha madogo. Lakini anajua Kombe la Dunia ni muhimu.”

Deschamps pia alikanusha mapendekezo kwamba kukosekana kwa Benzema hivi karibuni kwa Real Madrid kumekuwa ni jaribio la makusudi la kujiokoa ili aitumikie Ufaransa.

"Sio kwamba Benzema hakutaka kuichezea Real Madrid, hakuwa tayari. Lakini nina uhakika atakuwa tayari kwa Kombe la Dunia,” aliongeza kocha huyo.

Top Stories