Kubenea azua kizaazaa CCM

17Jan 2016
Taifa Letu
Kubenea azua kizaazaa CCM

USHINDI wa mbunge wa jimbo la Ubungo jijini Dar es Salaam, Saed Kubenea, umesababisha kusimamishwa kazi kwa kipindi cha miaka minne makatibu kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakituhumiwa kuhujumu chama hicho kwa kusaidia kampeni za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati wa uchaguzi mkuu uliopita na chadema kupata ushindi.

Saed Kubenea

Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana Kubenea wa Chadema alishinda nafasi hiyo dhidi ya Dk. Didas Masaburi wa CCM.

Kwa nafasi ya udiwani wa kata ya Manzese katika jimbo hilo ilichukuliwa na Ramadhan Kwangaya wa Chama cha Wananchi (CUF) aliyekuwa akichuana na Abdulkarim Atik wa CCM.

Kufuatia ushindi huo wa upinzani, CCM kata ya Manzese, jijini Dar es Salaam imewasimamisha kazi makatibu wanne wa matawi na waenezi wawili kwa muda wa miezi 48 sawa na miaka minne.

Kwa mujibu wa katibu wa CCM wa kata hiyo, Ramadhan Kidoga makatibu waliosimamishwa ni wa matawi ya Muungano, Mferejini na Uzuri Manzese, na Midizini huku akifafanua kuwa bado uchunguzi unaendelea ili kuwasimamisha wengine zaidi kwa kitendo cha kusaliti chama hicho na kusisitiza kuwa tayari wameshaandikiwa barua za kusimamishwa.
Aliwataja makatibu waliosimamiwa na kupatiwa barua kuwa ni pamoja na Gaudence Mapunda wa tawi la Muungano, Kifwebe Zanaki(Mferejini), Rashidi Mpehe (Uzuri Manzese), Joyce Ngalunda (Midizini), Hamisi Bakari ambaye ni katibu wa siasa na uenezi tawi la Uzuri Manzese na mmoja ambaye ni Katibu wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) pia kutoka tawi hilo Mangaza Shomari.
Taifa Letu lilibahatika kupata moja ya barua walizoandikiwa makada hao waliosimamishwa ambayo haina kumbukumbu namba ya Novemba 6, 2015 akielezea baadhi ya sababu za kusimamishwa kwao kama ilivyonukuliwa ikisema:
"Nasikitika kukuarifu kuwa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Kata katika kikao chake kilichoketi tahere 05/11/2015 kimeamua kukusimamisha nafasi ya uongozi wa Katibu wa Siasa na Uenezi na nafasi nyingine zote za chama ulizo nazo baada ya kuridhika kuwa umehusika kukisaliti chama wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,"ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Kidoga.
Barua hiyo inaeleza kuwa tangu awali baada ya kura za maoni za udiwani na ubunge, wakati wa kampeni, siku ya uchaguzi, makada hao kwa nyakati tofauti walikutwa wakihusika na vitendo vya kukihujumu na kukisaliti chama ili kishindwe udiwani na ubunge.
"Kamati ya Siasa ya Kata katika vikao vyake ilikuwa ilikuonya kwa mdomo ujirekebishe na kuachana na tabia hiyo ovu kwa chama lakini ukawa mkuu wa idara ya ushawishi, uhamasishaji na propaganda," ameandika Kidoga.
Tuhuma nyingine ni kuchelewesha kwa makusudi posho za wajumbe wa nyumba kumi zilizotolewa na chama makao makuu kwa ajili ya motisha ili kupita kwenye mashina yao kushawishi na kuhamasisha watu wao usiku wa kuamkia siku ya Uchaguzi Mkuu ili wapigie CCM.
Kwa mujibu wa Kidoga posho hizo zilifikishwa kwa walengwa baada ya uchaguzi kumalizika na kusababisha CCM kushindwa katika uchaguzi huo.
"Kwa mantiki hiyo huwezi ukaendelea kuwa kiongozi wa CCM, unasimamishwa uongozi kwa nafasi zote za chama ulizo nazo na kuwa chini ya uangalizi wa miezi 48," aliandika.
Akizunguza katika mahojiano na gazeti hili, mmoja wa watuhumiwa hao, Hamisi Bakari alisema tuhuma dhidi yake hazina ukweli wowote na kudai kuwa ni mbinu za katibu huyo kutaka kuficha ukweli baada ya kuboronga kwenye kura za maoni ndani ya chama.
"Ukweli ni kwamba Kidoga alikuwa na mgombea wake na hasa nafasi ya udiwani ambaye baadaye alishindwa na sasa anatafuta mchawi wakati yeye ndiye aliyesababisha hayo yote," alisema mmoja wa watuhumiwa hao.
Alisema kuwa katika kura za maoni kila mwanachama ana kundi lake na baada kupatikana mgombea wanaungana kwa ajili ya kukitetea chama, lakini katibu huyo bado anaendekeza makundi.
"Pamoja na kwamba amechangia chama kukosa kata kwa kulazimisha kuweka mtu wake, hata hali ha hewa katika Uchaguzi Mkuu haikuwa nzuri kwa CCM, watu wengi walikuwa wanataka mabadiliko," alisema na kuendelea:
"Ndio maana yapo baadhi ya majimbo kama Kibamba , sisi CCM hatuna kata hata moja, hivyo atambue hilo kwamba upepo haukuwa mzuri kwetu na pia hakuna aliyesaliti chama zaidi yake ambaye aliweka mgombea asiyekubalika. "
Alisema kuwa katibu huyo alikiuka taratibu za chama kwa kuandika barua za kuwasimamisha tangu Novemba 6, 2015 lakini akaja kuwapa Desemba 29, 2015 na kuwafanya wakose nafasi ya kukata rufaa.
"Binafsi ninachukulia barua hii kama mkakati maalum alioupanga kwa lengo la kutaka kuweka viongozi wanaomtii ili atakapowania tena nafasi hiyo katika uchaguzi ndani ya chama aweze kushinda kirahisi, lakini tutapambana naye," alisema.
Hadi tunakwenda mitamboni Kubenea wala kiongozi yeyote wa Chadema hakupatikana kuelezea madai hayo baada ya juhudi za kuwatafuta kugonga mwamba.

Top Stories