Familia yafunguka walivyoibiwa na mganga feki

23Feb 2024
Maulid Mmbaga
DAR ES SALAAM
Nipashe
Familia yafunguka walivyoibiwa na mganga feki

FAMILIA ya watu 16 inayodai kunyeshwa kitu kinachodhaniwa kuwa sumu na mtu aliyejifanya mganga wa kienyeji, imefunguka mengi yaliyojificha.

Tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita na kutolewa taarifa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP)  Jumanne Muliro, baada ya familia hiyo, yenye makazi Vijibweni, Kigamboni mkoani Dar es Salaam kukutwa mahututi.

Mwandishi wa habari hii alifika eneo la tukio na kuzungumza na dada mkubwa wa familia, Zenna Harisi, ambaye alisimulia chanzo cha tukio hilo na kubainisha kuwa  chanzo cha kukutana na mtu huyo ni mdogo wake ambaye anauza uji, aliyekwenda naye kama mteja.

Alisema baada ya kumuuzia (uji) wakati akiwa anakunywa, ndipo alipomwambia kuwa ana dawa za kuponya matatizo mbalimbali.

Zenna alisema baada ya mganga huyo kueleza hivyo ndipo mdogo wake akamwambia kuwa mama yake anasumbuliwa na miguu huko nyumbani. Alisema wawili hao walibadilishana namba na ndipo siku ya Jumapili alipokwenda nyumbani kwao.

“Alivyokuja alituuliza kuwa tuko tayari kwa ajili ya yeye kumshughulikia mama yetu tukasema ndiyo, akasema familia yote tukusanyike akawa anatengeneza dawa zake, kwanza akampa baba na wadogo zangu wa kiume na kike waende wakaoge.

“Baada ya hapo akasema mama anatatizo kwa hiyo lazima amtoe hicho kitu, akafanya kama mazingara fulani anayoyajua yeye, akatufunika na shuka, tukaona kuna kitu kakiangusha kama hirizi. Mara akasema hapo nje kuna kitu, akatuambia tutoke akamwambia mdogo wangu, ‘fukua hapo’ akatia maji, kikatoka kitu,” alisema.

Anaongeza: “Akaturudisha tena ndani akahesabu kama tulivyo pale akaomba gazeti kila mtu akachana kipande chake. Akachanganya dawa zake akatulambisha wote. “Alivyomaliza hapo akasema, wadogo zangu wawili anaona ndio wanamatatizo sana, bi mkubwa (akimaanisha mama) ameshamalizana naye ana afadhali.”

Zenna alisema wakati huo, dada yake alikuwa kama anagalagala chini na huyo mganga akadai kuwa mdudu ndo anamtoka. Alisema wakati akiendelea kufanya vitu vyake na wao dawa ikawa anazidi kuwalevya.

“Akatuuliza vyumba vyetu vilipo na kututaka twende tukalale. Alitupa bakuli ambayo imewekwa yai akasema, kila mtu akae chumbani kwake na akiwa anaangalia yai hilo kuna kitu tutakiona,” alisimulia Zenna.

Alisema kabla hajaingia chumbani aliambiwa akawaamshe watoto ambao pia, walilambishwa dawa na kuwaambia nao wakalale.

Alisema aliwachukua wazazi wao na kuwapeleka chumbani kwao na kuwaambia waendelee kuangalia mayai hayo na kila mtu ataona kitu kikitokea.

“Baada ya muda alikuja chumbani kwangu na kuniuliza kuwa, alimuona binti yangu ameshika simu kubwa iko wapi? Nikamwambia simu yake ninayo, kwani vipi? Akasema anataka kuipakaa dawa pia, lakini alivyotoka nikaichukua nikaidumbukiza kwenye tenga la nguo chafu.

“Aliporudi mara ya pili nilimuona kama mwenye mshangao, akaniuliza yaani wewe hadi sasa hivi hujalala? Nikamwambia nitalala vipi wakati umeniambia niangalie yai ndio nitaona matokeo nikilala itakuwaje?” alimhoji.

Alisema baada ya kumweleza hivyo, huyo mganga akamwambia asiwe na shida na kumtaka asinzie na majibu yatapatikana.

“Baada ya muda alianza kusinzia. Kumbe wakati huo mtu huyo alikuwa ameshaingia kwenye vyumba vingine na kuzima taa huku akipekuwa na kuiba fedha. Wakati huo wazazi na familia nzima tulikuwa hatujielewi,” alisimulia.

Ilipofika saa 10:00 usiku, alisema alishtuka usingizini na alipokwenda kuwaamsha watoto ili wajiandae kwenda shuleni, kila aliyemwamsha hakuamka zaidi ya kugalagala kitandani na baadhi kutapika.

Baada  ya tukio hilo alikwenda kwa majirani kuwaeleza na ndipo wakapata msaada wa kupelekwa hospitalini.

“Wakati huo yule mtu alikuwa ameshaondoka. Baba aliibiwa Sh. 450,000, dada Sh. 107,000 pamoja na simu sita kubwa tatu na ndogo nne. Hadi sasa watoto bado hawako sawa na hawajaanza kwenda shule,” alisema.

BABA AFUNGUKA

Baba wa familia hiyo, Harisi Amani, alisema tangu alipopatiwa dawa hizo amepatwa na tatizo la miguu kama mke wake na kushindwa kuendelea na shughuli zake za kila siku.

Alisema siku ya tukio alipewa dawa na kunawa uso na baada ya hapo akapata kizunguzungu.

“Nilipopelekwa chumbani nilimuona akiingia (chumbani) mara mbili na kila alipokuja alikuwa anatulazimisha tulale. Kama alirudi tena nilikuwa nimeshapoteza fahamu.

“Sikujua nini kiliendelea hadi fahamu iliponirudia nikajikuta niko hospitali ya Wilaya Kigamboni saa 7 mchana, shughuli zangu ni za baharini, lakini hadi sasa sina nguvu ya kufanya kitu chochote, hata chakula majirani ndio wanaotusaidia,” alisimulia Amani.

Amani alisema licha ya mtu huyo kuwafanyia kitendo hicho, amekuwa akituma ujumbe mfupi wa maandishi kwa ndugu ukitaka watume fedha akidai mzee yupo hospitalini anaumwa huku baadhi wakituma.

Katika taarifa yake, Kamanda Muliro alisema mtuhumiwa huyo bado anatafutwa na kuwataka wananchi kuwa makini na wimbi la matapeli wanaojifanya waganga wa kienyeji na kuishia kuiba.

Kamanda Muliro aliitaka jamii kuwafichua watu wanaowahisi kuwa wanajihusisha na aina hiyo ya utapeli ili wachukuliwe hatua za kisheria ikiwamo kufikishwa mahakamani.

 

 

 

Top Stories