Ajali hiyo ilitokea juzi majira ya saa 4.30 usiku eneo la Magila Gereza, Mombo Wilayani Korogwe, barabara Kuu ya Segera – Buiko mkoni Tanga.
Katika ajali hiyo, sanduku lililokuwa limebeba mwili wa marehemu lilivunjika na kubaki vipande vipande, hivyo mwili kupelekwa chumba cha maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe kuhifadhiwa.
Waliofariki dunia katika ajali hiyo ni ndugu 14 wa familia moja wakiwemo watoto wa marehemu, baba mkubwa, dada na baba mdogo.
Ndugu hao ni Lizybetha Lamesay, Elizabeth Mrema, Godwin Mrema, Kennedy Mrema, Athanas Mrema, Avelina Mrema, Emilian Lyakurwa, Agustina Mrema, Nestom Kiwango, Rozina Lamosai, Suzana Mrema, Julietha Mrema na Ethan Peter.
SAMIA AWALILIA
Kutokana na ajali hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema amesikitishwa na vifo vya watu hao.
“Nawapa pole wafiwa wote walioguswa na vifo hivi. Nawaombea ndugu zetu hawa wapumzike mahali pema na majeruhi wapone,” ulisomeka ujumbe wa Rais Samia katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
Aidha, Chama cha Wananchi (CUF), kilielezea kupokea kwa huzuni na masikitiko taarifa ya vifo hivyo.
“Chama kinatoa pole kwa wafiwa wote na kuwaombea majeruhi wapone haraka ili waendelee na majukumu yao ya kila siku. Lakini chama kinatoa wito kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia sheria na matumizi sahihi ya barabara ili kupunguza ajali na maafa yatokanayo na ajali hizo,” ilisema taarifa hiyo ya CUF.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba, alisema amepokea kwa masikitiko tukio la ajali mbaya iliyotokea usiku wa kuamkia jana na kusababisha uharibifu mkubwa wa magari hayo.
Mgumba alisema gari lenye usajili namba T.673 CUC, Mitsubish Fuso likiendeshwa na dereva ambaye jina lake halijafamika, liligongana na gari T.863 DXN Coaster iliyokuwa imebeba mwili wa marehemu na wanafamilia.
Alisema katika Coaster hiyo kulikuwa na abiria 26 waliotoka Dar es Salaam kwenda Rombo kwa mazishi ya ndugu yao.
Pia alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, majeruhi 10 wamehamishiwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tanga ya Bombo na wengine wawili wamebaki Korogwe.
Alisema chanzo cha ajali ni mwendokasi na uzembe wa dereva wa Mitsubishi Fuso aliyekuwa akijaribu kulipita gari la mbele bila kuchukua tahadhari, hivyo kugongana uso kwa uso na Coaster.
Baada ya kukaguliwa kwa ajali hiyo, Mgumba alisema magari hayo yameshaondolewa barabarani ili kuruhusu barabara kupitika.
MAJERUHI HALI MBAYA
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa waTanga ya Bombo, Dk. Naima Yusuph, alithibitisha kupokea majeruhi 12 jana majira ya saa 11:30 alifajiri na wanaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari wakisubiri ripoti ya daktari aliyewafanyia uchunguzi wa kina.

“Isipokuwa watano hali zao si nzuri na wawili inawezekana wakapatiwa rufani kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema Dk Yusuph huku akibainisha kuwa majeruhi hao walipokewa wakiwa na majeraha makubwa, hivyo kulazimika kupelekwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu.
HEMED ATEMBELEA MAJERUHI
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, aliwatembelea majeruhi hospitalini hapo na kuwapa pole. Kiongozi huyo aliambatana na Mgumba, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah na viongozi viongozi wengine wachama na serikali mkoani Tanga.
MASHUHUDA WASIMULIA
Shuhuda wa ajali hiyo, Gines Mrema, alisema marehemu Mrema (waliyekuwa wakienda kumzika) ni baba yake mdogo, alisema ndugu yao alikuwa anaishi Mbezi kwa Msuguri, alianza kuumwa na kufikishwa katika Hospitali ya Bochi kabla ya kufariki dunia.
Alisema juzi walienda kuuchukua mwili huo kwa ajili ya kuusafirisha kwenda Rombo Mkuu na wakiwa katika gari lililokuwa na wanafamilia wengi, walipata ajali ya kugongana uso kwa uso na Fuso eneo la Korogwe.
“Wamefariki (dunia) ndugu zetu 14 na wale wa fuso walikuwa watatu ukijumlisha na wa kwetu tunafikia idadi ya 17,” alisema.
Alibainisha kuwa katika ajali hiyo wamo watoto wawili wa marehemu wawili na upande wa baba yake wamefariki dunia dada yake aliyekuwa na watoto, baba mdogo na ndugu wengine.
Manusura mwingine wa ajali ambaye amelazwaBombo, Erick Edward Mrema, akizungumza namna ajali hiyo ilivyotokea, alisema wakati wanasafirisha mwili wa ndugu yao kwenda kuzika, walipofika eneo la Korogwe walikumbana na mkasa huo mzito.Alisema lilitokea lori na kuigonga Coaster waliyokuwa wamepanda na kuwapoteza ndugu zao 14 akiwamo dada yake aliyekuwa na mtoto.
Erick alisema kabla ya ajali hiyo, walikuwa na safari nzuri huku akisema katika safari hiyo, yeye alikaa nyuma pamoja na mtoto wake na anamshukuru Mungu wamenusurika.WAFIKA KUTAMBUA NDUGU
Ridhiwani Mbwambo ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kileo, Mwanga Mkoani Kilimanjaro alilazimika kufunga safari kufika Jijini Tanga kutafuta ndugu zake wawili na tayari amempata mmoja.Alisema baada ya kusikia taarifa za ajali hiyo, aliamua kufunga safari kukimbilia Hospitali ya Magunga, Korogwe kusaka ndugu zake na alipowakosa akaenda Bombo.
Daktari wa Dharura Bombo, Dk. Arafa Abubakar, alisema majeruhi waliopokewa wanaendelea vizuri isipokuwa wawili waliumia vibaya kichwani na watapewa rufani kwenda Muhimbili.
KUZIKWA JUMATATU
Msemaji wa familia na kaka mkubwa wa marehemu Atanas Mrema (59), Colman Mrema, alisema wamepata msiba mzito na baada ya kikao wamekubaliana kuzika Jumatatu kwa baadhi ya wanafamilia.
Alisema marehemu Mrema alikuwa na watoto sita, wa kiume wakiwa watano, wa kike mmoja, ambaye amefariki dunia katika ajali hiyo.
Aliishukuru serikali ya wilaya ambayo alisema imeahidi kuwapatia usafiri wa kufikisha miili yote katika maeneo ambayo watafanya mazishi.
*Imeandikwa na Oscar Assenga (Tanga), Mary Mosha (Rombo), Godfrey Mushi (Arusha) na Beatrice Shayo (Dar).




.jpeg?itok=vCj6bCRe)






