Matumizi ya mbegu na viuatilifu bado yapo chini sana

13Dec 2023
Ashton Balaigwa
MOROGORO
Nipashe
Matumizi ya mbegu na viuatilifu bado yapo chini sana

CHAMA cha Taaluma ya Sayansi Kilimo Mazao Tanzania (CROSAT), kimesema bado matumizi ya mbegu bora na matumizi sahihi ya viuatilifu yapo chini hivyo kina kusudia kuja na mkakati mpya utakaosaidia kuongeza matumizi hayo kwa wakulima ili wapate tija katika sekta ya kilimo hapa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Morogoro kuhusu kufanyika kwa mkutano mkuu wa mwaka, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Patrick Ngwediagi amesema kwa sasa matumizi ya mbegu bora na viuatilifu sio makubwa sana.

Amesema lengo la chama hicho ni kuwezesha wakulima walio wengi waweze kutumia mbegu bora zinazotokana na aina bora za mbegu.

Ngwediagi amesema kupitia mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika Dodoma Desemba 19-20 mwaka huu watalaam watawasilisha hali halisi ya mbegu nchini na kujadi kwa kina namna ya kuongeza uzalishaji mbegu bora kwa lengo la kujitosheleza.

“Sisi kama watalaam tunaenda kujadili kwa mapana namna kuongeza uzalishaji wa mbegu bora na upatikanaji wa mbegu na mifumo inayotumika kuhakikisha kwamba tunapata mbegu bora na tunatakuja na mkakati na mapendekezo ya kushauri kwa serikali,” amesema Ngwediagi.

Amesema mkutano pia utajali namna matumizi bora ya viatilifu kutokana na kuonekana hakuna matumizi sahihi ya viatilifu na kuchangia madhara kwa wakulima wenyewe kutokupata matokeo yanayokusudiwa.

“Mfano mkulima anaweza kutumia kiuatilifu ambacho kilikusudiwa kitumike kwa ugonjwa mwingine,au mdudu mwingine akatumia kwa ugonjwa usio kusudiwa akifikiri kila kiuatilifu kinatibu mmea na matokeo yake kupata hasara” amesema Ngwediagi.

Amesema matumizi yasiyo sahihi ya viatilifu yanaweza kuleta madhara kwa afya ya walaji hapa nchini na inaweza kuzuia kuzuiwa kusafirisha mazao ya kilimo nje ya nchi kwakuwa mazao yanayopokelewa nje yamekuwa yakifanyiwa vipimo kabla ya kuingizwa sokoni.

Naye Katibu Msaidizi wa CROSAT, Dk. Yasinta Nzogela,akizungumzia kuhusu ushiriki wa wanawake,alisema katika chama hicho wanawake wamehamasika kujiunga kutoka,Taasisi za Kitaaluma kama Vyuo vikuu,Vyuo vya Kati na kwamba wanaendelea kuhamasisha wanawake wa serikali za mitaa.

Dk. Nzogela aliwataja wanawake wengine ni kutoka sekta binafsi wanaomiliki makampuni ya sekta ya kilimo,wanaomiliki mashamba ili waweze kunufuika kwa kupata elimu sahihi mawazo chanya tofauti katika kuendeleza shughuli zao kilimo.

Top Stories