Kiiza baba we noma!

24Jan 2016
Lete Raha
Kiiza baba we noma!

HAMIS Kiiza amefunga mara mbili na kuisaidia timu yake ya Simba kutinga raundi ya nne ya Kombe la Shirikisho kufuatia ushindi wa 3-0 dhidi ya Burkinafaso ya Morogoro.

Hamis Kiiza

Ilikuwa ni mechi ya tatu mfululizo chini ya kocha mpya Jackson Mayanja na ushindi wa tatu mfululizo kwa Mganda huyo aliyerithi mikoba ya Muingereza Dylan Kerr aliyetimuliwa Msimbazi.
Simba walilazimika kusubiri hadi dakika ya 77 kupata bao la kwanza, wakati Kiiza alipounganisha kwa kisigino mpira wa krosi iliyomiminwa ndani ya boksi na Banda kutoka wingi ya kushoto kaskazini mwa Uwanja wa Jamhuri.
Ndemla aliyekuwa hatua mbili kutoka kwenye boksi la Bukinafaso, alitupia la pili kwa shuti kali la kimo cha mbuzi kwa mguu wa kulia katika dakika ya 90+2.
Wakati mashabiki wakiamini mechi hiyo ingemalizika kwa matokeo ya 2-0, Ndemla alikwatuliwa ndani ya boksi na Kiiza alimchambua kwa shuti la kimo cha panya kwa mguu wa kulia penalti iliyoamuliwa na refa Andrew Shamba katika dakika ya 90+4.
Kung'ara kwa Mganda huyo (25), kunazidi kuwaamiza mashabaki wa Yanga kwani mkali huyo wa mabao alitemwa na uongozi wa Jangwani Desemba 2014 akidaiwa kushuka kiwango, lakini sasa anakamata nafasi ya pili kwenye orodha ya wafumania nyavu hatari wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu akiwa na magoli 10, matatu nyuma ya kinara, Amissi Tambwe wa Yanga.

Top Stories