Wasugua benchi kuteka kikosi cha Simba Mapinduzi

02Jan 2016
Nipashe Jumapili
Wasugua benchi kuteka kikosi cha Simba Mapinduzi

WAKATI timu ya Simba inatarajia kutua visiwani Zanzibar leo kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, kocha wa timu hiyo, Dylan Kerr, amesema kikosi chake kitasheheni wachezaji ambao wamekuwa wakisugua benchi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu.

Kikosi cha Simba

Michuano ya 10 ya Kombe la Mapinduzi inaanza rasmi leo kwa mechi mbili za Kundi B zikizikutanisha Yanga na Mafunzo FC ya Zanzibar kwenye Uwanja wa Amaan saa 10:15 jioni kabla Mtibwa Sugar kuchuana na Azam FC uwanjani hapo saa 2:15 usiku.
Simba wataanza kutetea taji lao kesho kwa kuikabili Jamhuri FC ya Zanzibar saa 2:15 kwenye Uwanja wa Amaan, wakitanguliwa na mechi ya kwanza ya Kundi A kati ya JKU FC ya Zanzibar na URA ya Uganda.
Akizungumza na gazeti hili mjini hapa kabla ya kuanza safari ya kurejea Dar es Salaam jana asubuhi, Kerr (48) alisema kutetea ubingwa ni jambo ni jambo muhimu, lakini kusuka kikosi imara kwa ajili ya Ligi Kuu ni muhimu zaidi.
Kutokana na kuwa na mwenendo wa kusuasua msimu huu, beki huyo wa zamani wa Leeds United alisema kikosi chake cha Kombe la Mapinduzi mwaka huu kitakuwa na wachezaji ambao hawajapata nafasi kubwa ya kucheza katika mechi 13 zilizopita za VPL msimu huu.
"Tunahitaji kutetea ubingwa wetu (Kombe la Mapinduzi), lakini muhimu zaidi ni kwamba tunapaswa kuwapa nafasi wachezaji wetu ambao hawajapata fursa ya kuonyesha uwezo wao Ligi Kuu msimu huu," alisema.
"(Mohamed) Fakh, (Paul) Kiongera, (Brain) Majwega, wanapaswa kupewa nafasi kikosini ili watuonyeshe uwezo wao. Jumapili (leo) tutakwenda Zanzibar, sijajua idadi ya wachezaji ambao tutaondoka nao."
Simba ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo mwaka jana ikiwa chini ya Mserbia Goran Kopunovic ilikiibwaga Mtibwa Sugar katika hatua ya matuta baada kutoka suluhu kwenye muda wa kawaida.
Wekundu wa Msimbazi ndiyo timu iliyotinga hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi mara nyingi zaidi. Imefika fainali mara tano 2008, 2011, 2012, 2014 na 2015 ikifuatwa na Mtibwa Sugar waliotinga fainali mara nne 2007, 2008, 2010 na 2015. Yanga imefika fainali mara mbili 2007 na 2011 ikitwaa taji hilo mara moja 2007 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Top Stories