SERIKALI imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma, ambao unalenga kuondoa tatizo la malimbikizo ya stahili zao.
Hayo yalisema juzi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana alipozungumza na watumishi wa sekta mbalimbali katika wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu.
Waziri Mkuu alisema mfumo huo ujulikanao kama LAWSON, unatumika kwenye ajira za watumishi wote wa serikali kuu na wale wa serikali za mitaa nchini.
Waziri Mkuu alisema mfumo huo unasaidia kutunza, kutuma na kuhuisha taarifa za watumishi kwa wakati na kwa ufanisi tangu mtu anapoajiriwa hadi inapofikia wakati wa kupandishwa madaraja na hadi anapostaafu.
Kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo, maofisa utumishi walipaswa kukusanya taarifa za watumishi wote walioajiriwa na kuzipeleka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili zikathibitishwe kabla ya kuzipeleka Hazina kwa maandalizi ya mishahara.
Akitolea mfano wa kada ya ualimu, Waziri Mkuu alisema ajira za walimu zilikuwa zinaanzia Idara ya Utumishi wa Walimu (TSD) lakini anapaswa aende kuripoti kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED) ambaye ni mwajiri wake chini ya Tamisemi.
"Hii ilileta ugumu wa malipo ya kupanda madaraja, uhamisho au likizo kwa sababu mwajiri anakuwa hajatenga hizo fedha. Sasa hivi tuna Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) ambayo iko chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri. Kwa hiyo ni rahisi wao kukaa na kuamua tuwapandishe daraja walimu 10 na wote hao wakalipwa bila kuchelewa," alisema.
Alisema mfumo huo umeanza kutumika tangu mwaka 2012 na ulianza kwa ajira mpya za walimu. Alisema hadi sasa umethibitisha kuwa inawezekana kumlipa mtumishi mshahara wake hata kama ameajiriwa ndani ya mwezi huo huo.
"Kama mtumishi anaripoti kwenye kituo kipya hata iwe wilaya ya wapi ili mradi amefika na barua zake zote na ziko sahihi mtu huyu ataingiziwa taarifa zake na wakati huo huo taarifa zitaonekana Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na pia zitapokewa kwa maofisa wanaoshughikia mishahara kule Hazina," alisema.
Hata hivyo, alisema changamoto pekee waliyokutana nayo wakati mfumo huo umeanza ilikuwa kutoingizwa taarifa za wale ambao wameripoti baada ya tarehe 10 ya mwezi husika.
ooooo