Katambi atamba kutekeleza ahadi aliahidi kwa wananchi Shinyanga

14Mar 2024
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Katambi atamba kutekeleza ahadi aliahidi kwa wananchi Shinyanga

MBUNGE wa Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, amesema ahadi ambazo aliwahidi wananchi kipindi cha uchaguzi Mkuu 2020 nyingi amezitekeleza na kuwaletea maendeleo wananchi wa Shinyanga.

Mbunge wa Shinyanga Mjini Patrobas Katambi akizungumza na wananchi wa Kitangili kwenye Mkutano wa hadhara.

Katambi amebainisha hayo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Kitangili kwenye Mkutano wa hadhara.

Katambi ambaye pia Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye ulemavu, amesema kutokana na machungu aliyonayo kwa wananchi wa Shinyanga, amekuwa akitafuta fedha ili kuteleza miradi mingi ya maendeleo,na kwamba ahadi ambazo alikuwa ameahidi nyingi ameshazitekeleza.

"Ahadi ambazo niliwahidi wananchi kipindi cha uchanguzi nyingi nimetekeleza na ninamshukuru Rais Samia kwa kuniunga mkono kero nyingi zimetatuliwa ikiwamo miundombinu ya barabara ambayo ilikuwa korofi na madaraja," amesema Katambi.

"Mimi namapenzi mema na wananchi wa Shinyanga, siyo mtu wa starehe mfano fedha za jimbo za mwaka jana Sh. milioni 61.6 nimezigawa zote kwenye Kata ili zikatekeleze miradi ya maendeleo, ningekuwa na tamaa ya fedha si ningekula," ameongeza Katambi.

Aidha, Katambi ameeleza kuchukizwa na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiwapiga majungu viongozi na kuwafanya fitina za ajabu ikiwamo yeye kwamba afukuzwe katika nafasi ya Naibu Waziri, nakuwataka waache tabia hiyo bali waungane kuwaletea maendeleo wananchi.

Diwani wa Kitangili Mariamu Nyangaka, amemshukuru Katambi pamoja na Rais Samia kwa kumuunga mkono na kufanikisha ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja ambayo yalikuwa kero kubwa za wananchi, huku akiahidi kuendelea kumalizia kero zilizobaki.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Anorld Makombe, ametoa wito kwa wananchi kwamba kutokana na kasi kubwa ya maendeleo ambayo wameletewa wawaunge mkono viongozi wote wa CCM na kuwapigia kura kwa wingi katika chaguzi zijazo.

Katika ziara hiyo ya Katambi ameambatana pia na Madiwani wote wa Manispaa ya Shinyanga na kuelezea utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa wananchi.